Saturday, October 16, 2010

Kura mpya ya maoni: Dk. Slaa ampiku JK
•  Wazee wengi ni wa Kikwete, vijana wa Dk. Slaa

na Bakari Kimwanga
 
 
KURA nyingine ya maoni iliyoendeshwa na taasisi ya Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB) inaonyesha kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ndiye mgombea anayekubalika zaidi katika uchaguzi wa mwaka huu kuliko mwingine yeyote.
Matokeo ya kura hiyo ya maoni yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam yanaonyesha kuwa Dk. Slaa alikuwa ndiye mgombea aliyekuwa akipewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda urais mwaka huu na ambaye pia angepigiwa kura na watu wengi zaidi waliohojiwa katika utafiti huo.
Akitangaza matokeo ya kura hiyo ya maoni katika Hoteli ya Courtyard, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Vincent Leyaro, alisema utafiti huo ulikusanya maoni ya wananchi katika mikoa 15 ya Tanzania Bara kwa kuchagua jimbo moja kila mkoa, kata mbili mbali na vijiji na mitaa miwili katika majimbo husika.
Dk. Leyaro alisema miongoni mwa watu 3,047 waliohojiwa katika utafiti huo ulioendeshwa katika kipindi cha kati ya Septemba 27 na Oktoba 10, asilimia 48 walimpa Dk. Slaa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete akipata asilimia 38 na nafasi ya tatu ikishikwa na Profesa Ibrahimu Lipumba anayegombea kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) ambaye alitajwa na asilimia 9 ya waliopiga kura hiyo ya maoni.
Mbali ya hilo, utafiti huo uliwauliza waliohojiwa iwapo uchaguzi ungefanyika siku walipohojiwa wangemchagua mgombea gani kuwa rais, asilimia 45 walimtaja Dk. Slaa, asilimia 41 wakisena watampigia kura Kikwete na asilimia 10 wakimtaja Profesa Lipumba.
Matokeo hayo ya TCIB, taasisi inayojumuisha wanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yanamfanya Rais Kikwete kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano kuporomoka kutoka katika kuongoza kura za maoni hadi kushika nafasi ya pili nyuma ya mgombea kutoka kambi ya upinzani.
Akiendelea kueleza namna walivyofanya utafiti wao, Dk. Leyaro alisema katika washiriki wote 3047 waliohojiwa, asilimia 18.3 walisema wao ni wanachama au mashabiki wa CCM, wakati asilimia 15.6 walijitanabahisha na CHADEMA na asilimia 12 wakijifungamanisha na CUF.
Mbali ya hao watafiti hao walisema asilimia 31. 6 ya watu wote waliohojiwa walijitaja kuwa watu ambao hawakuwa wanachama au mashabiki wa chama chochote cha siasa miongoni mwa vyama 18 vilivyo katika daftari la msajili wa vyama.
Katika uchambuzi wa upigaji kura kwa mtazamo wa vyama, matokeo ya kura hizo za maoni yalionyesha kuwa asilimia 72 ya watu waliohojiwa ambao walisema walikuwa hawafungamani na chama chochote cha siasa walimtaja Dk. Slaa kuwa ndiye chaguo lao, akafuatiwa kwa mbali na Kikwete aliyepata asilimia 11 na Lipumba akapata asilimia 10.
Katika eneo jingine kura hiyo ya maoni inaonyesha kuwa wakati Kikwete anaungwa mkono na asilimia 80 ya wapiga kura wa ndani ya CCM, Dk. Slaa alikuwa akiungwa mkono na asilimia 90 ya wana CHADEMA huku Lipumba akiungwa mkono na asilimia 38 ya mashabiki na wanachama wa CUF.
Utafiti huo ulitoa matokeo mengine ya kushangaza baada ya kuonyesha kwamba asilimia 15 ya wanachama na wapenzi wa CCM walikuwa wakimuunga mkono Dk. Slaa wa CHADEMA huku wana CUF wafikao asilimia 48 wakimuunga mkono Kikwete badala ya mgombea wao wa urais, Profesa Lipumba.
Dk. Leyaro alisema utafiti huo pia ulifanya uchambuzi wa wahojiwa kirika na kubaini kuwa vijana wengi zaidi miongoni mwa waliohojiwa walisema watamchagua Dk. Slaa, huku sehemu ya kundi la watu wa umri wa zaidi ya miaka 50 likisema kuwa litamchagua Kikwete.
“Tulipofanya uchambuzi kwa makundi ya umri wa wahojiwa, ilijitokeza kuwa vijana wengi walimchagua mgombea wa CHADEMA (Slaa) wakati wahojiwa wa umri wa zaidi ya miaka 50 walimchagua mgombea wa CCM,” alisema Dk. Leyaro.
Katika eneo hili, utafiti huo ulibainisha kwamba asilimia 25 ya wahojiwa wenye umri wa chini ya miaka 25 walisema watamchagua Kikwete wakati asilimia 55 ya waliohojiwa wenye umri wa miaka chini ya miaka 50 walisema watamchagua Dk. Slaa.
Utafiti huo ulionyesha pia kwamba kwa wahojiwa wenye umri wa kati ya miaka 46 na 55 asilimia 50 walisema watamchagua Kikwete huku watu wa kundi hilo wapatao asilimia 35 wakimtaja Dk. Slaa, hali inayoonyesha kwamba mgombea wa CCM alikuwa akiungwa mkono zaidi na wagombea wenye umri mkubwa na wazee wakati Dk. Slaa akiungwa mkono zaidi na vijana na watu wenye umri wa kati.
Kwa upande wa mikoa na namna wagombea hao walivyoonekana kuungwa mkono, Kikwete aliongoza kwa kupata kura nyingi kuliko wengine katika mikoa ya Dodoma (59.3%), Lindi (43.4%) Mbeya (50%), Rukwa (54.3%), Ruvuma (55%) na Tabora (42%).
Wakati Kikwete akiongoza katika mikoa hiyo sita, Dk. Slaa yeye aliongoza katika mikoa minane ya Arusha (60%), Dar es Salaam (42%), Iringa (58.2), Kagera (49%), Kilimanjaro (71%), Mara (54%), Manyara (79.8%) na Mwanza (42.1%) huku Profesa Lipumba akiwa haongozi katika mkoa wowote na akafanikiwa kushika nafasi ya pili katika mkoa mmoja tu wa Lindi (38.1%).
Hata hivyo Dk. Leyaro, alisema kuwa matokeo hayo ni kura ya maoni sio lazima yawe taswira halisi ya siku ya kupiga kura na kusisitiza kuwa hali halisi ya matokeo itajulikana baada ya wananchi kupiga kura katika uchaguzi ulio huru na haki.
Alisema taasisi hiyo haitarajii wagombea na wapiga kura wao kubweteka au kukata tamaa kwa sababu ya matokeo ya kura za maoni na kutoa changamoto kwa kufanywa mara nyingi kwa kura hizo za maoni na mashirika mengi ambayo ni huru yasiyoegemea upande wowote.
Hata hivyo alisema matokeo hayo yanaweza kusaidia wagombea kujikita vizuri katika muda wa kampeni uliobaki kwa kuzingatia wapi wanakubalika zaidi na makundi gani ili waweze kuelekeza nguvu zao ipasavyo katika muda wa kampeni.
Wiki chache zilizopita taasisi ya Synovate ikionyesha mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Slaa, kupanda kwa alama nne, huku mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, akishuka kwa alama 10.
Matokeo hayo yalipishana na yale yaliyotolewa na taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) ambayo ilimpa Kikwete asilimia 71.2, Dk. Slaa (12.3) na mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (10.3).
Source:Mtanzania Daima.