Katika eneo hili, utafiti huo ulibainisha kwamba asilimia 25 ya  wahojiwa wenye umri wa chini ya miaka 25 walisema watamchagua Kikwete  wakati asilimia 55 ya waliohojiwa wenye umri wa miaka chini ya miaka 50  walisema watamchagua Dk. Slaa.  
Utafiti huo ulionyesha pia kwamba kwa wahojiwa wenye umri wa kati  ya miaka 46 na 55 asilimia 50 walisema watamchagua Kikwete huku watu wa  kundi hilo wapatao asilimia 35 wakimtaja Dk. Slaa, hali inayoonyesha  kwamba mgombea wa CCM alikuwa akiungwa mkono zaidi na wagombea wenye  umri mkubwa na wazee wakati Dk. Slaa akiungwa mkono zaidi na vijana na  watu wenye umri wa kati.  
Kwa upande wa mikoa na namna wagombea hao walivyoonekana kuungwa  mkono, Kikwete aliongoza kwa kupata kura nyingi kuliko wengine katika  mikoa ya Dodoma (59.3%), Lindi (43.4%) Mbeya (50%), Rukwa (54.3%),  Ruvuma (55%) na Tabora (42%).
Wakati Kikwete akiongoza katika mikoa hiyo sita, Dk. Slaa yeye  aliongoza katika mikoa minane ya Arusha (60%), Dar es Salaam (42%),  Iringa (58.2), Kagera (49%), Kilimanjaro (71%), Mara (54%), Manyara  (79.8%) na Mwanza (42.1%) huku Profesa Lipumba akiwa haongozi katika  mkoa wowote na akafanikiwa kushika nafasi ya pili katika mkoa mmoja tu  wa Lindi (38.1%).
Hata hivyo Dk. Leyaro, alisema kuwa matokeo hayo ni kura ya maoni  sio lazima yawe taswira halisi ya siku ya kupiga kura na kusisitiza kuwa  hali halisi ya matokeo itajulikana baada ya wananchi kupiga kura katika  uchaguzi ulio huru na haki.
Alisema taasisi hiyo haitarajii wagombea na wapiga kura wao  kubweteka au kukata tamaa kwa sababu ya matokeo ya kura za maoni na  kutoa changamoto kwa kufanywa mara nyingi kwa kura hizo za maoni na  mashirika mengi ambayo ni huru yasiyoegemea upande wowote.
Hata hivyo alisema matokeo hayo yanaweza kusaidia wagombea kujikita  vizuri katika muda wa kampeni uliobaki kwa kuzingatia wapi wanakubalika  zaidi na makundi gani ili waweze kuelekeza nguvu zao ipasavyo katika  muda wa kampeni.
Wiki chache zilizopita taasisi ya Synovate ikionyesha mgombea urais  kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Slaa,  kupanda kwa alama nne, huku mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya  Kikwete, akishuka kwa alama 10.
Matokeo hayo yalipishana na yale yaliyotolewa na taasisi ya Utafiti  na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) ambayo ilimpa Kikwete asilimia  71.2, Dk. Slaa (12.3) na mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (10.3).