Na: Lilian Lundo-MAELEZO Dodoma.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote Nchini kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato kuanzia Julai 01, 2016.
Majaliwa aliyasema hayo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akihitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja Juni 30, 2016.
"Napenda kutumia fursa hii kuziagiza Halmashauri zote Nchini kwamba kuanzia tarehe Mosi Julai, 2016 zihakikishe zinatumia mifumo ya kieletroniki katika kukusanya mapato, katika kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboreshha makusanyo," alifafanua Mhe. Majaliwa
Aidha Majaliwa amezitaka Halmashauri hizo kutoelekeza vyanzo vyote vya mapato kukusanywa na mawakala kwani vipo vyanzo ambavyo vinaweza kukusanywa kwa ufanisi na Halmashauri zenyewe bila kutegemea mawakala.
Aliendelea kusema kuwa, Halmashauri zitaelekezwa kwa waraka ni vyanzo vipi vitahitaji kutumia mawakala na vingine vitakusanywa na Halmashauri zenyewe kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Serikali.
Majaliwa aliitaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Halmashahuri aidha kwa kutumia mawakala au Halmashauri zenyewe kuweka kwenye akaunti ya Halmashauri fedha zote zinazokunywa kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ili kupunguza na kumaliza kabisa masuala ya (cash transactions).
Vile vile Halmashauri zikubaliane na wakala ni kiasi gani cha asilimia ya makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo yafanyike baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.
Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura 290, inazipa uwezo mamlaka za Serikali za Serikali za Mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada mbalimbali kama vyanzo vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Sheria hiyo pia inazipa mamlaka hizo kuteua Mawakala wa kukusanya mapato hayo kwa niaba ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.