Sunday, June 12, 2016

WATANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUPIGA VITA MATUKIO YA MAUAJI



WATANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUPIGA VITA MATUKIO YA MAUAJI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania, viongozi wa dini zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita matukio maovu ya mauaji yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema anatarajia hali ya amani, usalama na utulivu inaendelea kuwepo nchini, hivyo wananchi hawana budi kushirikiana na kushikamana na Serikali katika kuhakikisha matendo maovu hayatokei katika maeneo yao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati  alipowasili mkoani Geita kwa ajili ya kuhudhuria ibada ya kuwekwa wakfu Padre Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.

"Mfano tukio la Mwanza watu wanavaa kanzu na wanaingia msikitini na kukuta wenzao wanafanya ibada kisha wakawachinja, hii haiwezekani kwa binadamu wa kawaida hivyo tushirikiane katika kupiga vita matendo haya," alisisitiza.

Hivi karibuni jumla ya watu 15 waliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga katika mikoa ya Mwanza,Tanga, Dar es Salaam  na Mara.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga amesema vitendo vya watu kuuawa kwa kukatwa mapanga vimepungua baada ya kuanzisha kampeni maalumu ya kukemea mauaji hayo.

Alisema katika kampeni hiyo wameamua kuwatumia walimu, viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wauguzi ambao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina na badala yake wajikite katika masuala ya maendeleo.