Katika kuhakikisha kunakuwa na wasomi ambao wanakuwa na elimu kuhusu kodi, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imefanya uzinduzi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kodi (Student Tax Association) katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambapo wanachama hao watatumika kutoka elimu kwa wananchi wengine kuhusu kodi.
Akizungumza katika uzinduzi wa jumuiya hiyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema malengo ya kuwa na jumuiya za kodi vyuoni ni kuwezesha jamii kupata elimu ya kutosha kuhusu kodi kupitia wanachama wa jumuiya hizo ambao watakuwa wakipatiwa mafunzo kuhusu umuhimu wa kulipa kodi lakini pia kuhudhulia midahalo mbalimbali ambayo itakuwa inazungumzia kodi.
Alisema hatua ya kuanzisha jumuiya hizo imekuja baada ya kuwa na vilabu katika shule za msingi na sekondari nchini na sasa wakaona kuna umuhimu wa kuwa na wanachama kutoka vyuo vya elimu ya juu ili wawe mabalozi wa TRA ili kusaidia utoaji wa taarifa kuhusu kodi lakini pia na wao kutambua umuhimu wa kodi ili hata baada ya masomo yao waweze kuwa walipa kodi wazuri.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kodi chuoni hapo (Student Tax Association).
"Tulianzisha mfumo wa vilabu mwaka 2008 ambapo tuna vilabu 195 kwa Tanzania Bara na Zanzibar na katika vilabu hivyo tuna wanachama 15,520 hivyo tukaona sasa ni muhimu kuwa na wanachama kutoka vyuoni ili nao waweze kupata elimu kuhusu kodi,
"Wanachama wa jumuiya hizi watakuwa na shughuli ya kutoa elimu kwa watu wengine ambao hawana elimu ya kodi, kuandaa wataalum wa elimu ya kodi kwa miaka ya baadae na hata walipa kodi wa baadae kwani tayari watakuwa wanafahamu umuhimu wa kodi kwa maendeleo ya taifa," alisema Kayombo.
Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kodi IFM (ISTA), Amon Ojode akielezea jinsi ambavyo wanafunzi wa IFM watanufaika na uwepo wa jumuiya hiyo chuoni hapo.
Nae Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kodi IFM, Amon Ojode alisema kuwa ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wa chuo hicho kupata nafasi ya kuwa na jumuiya ya kodi na zaidi ni wanafunzi ambao wanajifunza masomo yanayohusiana na kodi hivyo wanaamini watakuwa wawakilishi wazuri wa TRA.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kodi chuoni hapo (Student Tax Association).
Waziri wa Afya na Mambo Yote kwa Ujumla katika serikali ya wanafunzi wa IFM (IFMSO), Suleiman Kahumbu akizungumza katika uzinduzi huo.
Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Diana Masalla akizungumzia kodi wakati wa uzinduzi wa jumuiya hiyo.
Baadhi ya wanachama wa Jumuiya wa Wanafunzi wa Kodi IFM na wanafunzi wa chuo hicho waliohudhuria uzinduzi wa jumuiya chuoni hapo.