Tukio hilo limetokea leo majira ya asubuhi muda mfupi baada ya Profesa Tibaijuka kufungua mkutano wa Kimataifa unaohusu upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira, mkutano unaoendelea jijini Dar es Salaam ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.
Profesa Tibaijuka ni Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kimataifa la Ushirikiano wa Upatikanaji wa Maji Safi na Salaam lijulikanalo kwa kifupi kama WSSCC ambalo pamoja na mambo mengine ndiyo linalohusika na mfuko wa dunia wa ufadhili wa miradi ya maji ambao unafadhili miradi kadhaa ya upatikanaji wa maji katika wilaya kadhaa za mkoa wa Dodoma.
EATV imefanikiwa kuzungumza na Profesa Tibaijuka ili kufahamu sababu za kutumia usafiri huo unaoonekana kutumiwa zaidi na watu wa kipato cha chini na haya yalikuwa majibu yake "Unajua mimi ni mbunge, ukiwa mbunge ni mwakilishi wa watu kwa hiyo sina tofauti yoyote na wale watu ninaowawakilisha," amesema Profesa Tibaijuka.
Ameongeza kuwa " sasa hivi natakiwa kuwahi ndege uwanja wa ndege kwenda mjini Dodoma kuhudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea huko kwa hiyo badala ya kutumia usafiri wangu ni bora nitumie hii bajaj ambayo kwa kweli ni msaada sana pale unapotaka kuwahi mahali,"
Idadi kubwa ya wageni waliohudhuria mkutano huo ambao wengi ni kutoka nje ya nchi hawakuamini kile kilichokuwa kikitokea kwani ni nadra kwa kiongozi wa hadhi yake ambaye amewahi kushika nyadhifa kubwa ndani ya Umoja wa Mataifa na taasisi mbali mbali za kimataifa kutumia usafiri unaoonekana kama ni wa hadhi ya chini.
"Huyu kweli ni kiongozi wa watu, mengi yanaweza kusemwa lakini huyu anaonyesha utu na upendo kwa watu anaowaongoza," alisikika mshiriki mmoja akisema kwa mshangao na kuongeza kuwa hata miradi ya maji iliyotekelezwa chini ya uongozi wake,jimboni kwake na hata mkoani Dodoma inaonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
Awali katika mkutano huo, Profesa Tibaijuka amesema suala la upatikanaji wa majisafi na salama ni muhimu iwapo nchi inahitaji kutokomeza umaskini na kwamba wananchi wanachotakiwa kufanya ni kuzingatia usafi wa mazingira na miili yao kwa kufuata kanuni za afya bora.
Profesa Tibaijuka ameongeza kuwa "Wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa umaskini sio chanzo cha uchafu bali ni tabia ya mtu..hivyo basi licha ya umaskini tulionao kama taifa sio sababu ya uchafu kutawala majumbani kwetu na kuwa chanzo cha magonjwa....kuna haja ya jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na rais Dkt John Pombe Magufuli za kutokomeza uchafu katika jamii kwani kama kiongozi wa nchi yeye mwenyewe ameonekana akichukia uchafu kwa vitendo,"
Kwa upande wake, Mratibu wa Baraza hilo hapa nchini, mhandisi Wilhelmina Malima amesema Tanzania inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye miradi ya maji safi na salama na hivyo kuiwezesha kutekeleza lengo namba sita kati ya malengo kumi na saba endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo hujulikana kwa kiingereza kama Sustainable Development Goals au kwa kifupi SDGs.