Sunday, April 10, 2016

WAZIRI MBARAWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA FLOW METER.



WAZIRI MBARAWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA FLOW METER.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mtambo mpya wa kisasa wa kupima mafuta yanayoingia nchini flow meter unaojengwa Kigamboni jijini Dar es salaam uko katika hatua za mwisho za kukamilika kwake na utaanza kazi rasmi mapema mwezi ujao.

Prof. Mbarawa amesema hayo wakati alipokagua mtambo huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na kuhimiza waendeshaji wa mtambo huo wawe watu wenye uadilifu wa hali ya juu na elimu ya kutosha ili kuulinda na kuwezesha kufanyakazi inavyostahili.

"Hakikisheni mnawasiliana na Wakala wa Vipimo nchini (WMA), ili wahakikishe mtambo huu unaviwango vinavyotakiwa vitakavyowawezesha wafanyabiashara wa mafuta kuridhika na ufanyakazi wa mtambo huu ili kuondoa malalamiko", amesema Prof. Mbarawa.

Zaidi ya shilingi bilioni 12 zimetumika katika ujenzi wa mtambo huo ambao utawezesha Serikali kupata mapato stahiki na wafanyabishara kupata mafuta sahihi kwa mujibu wa mahitaji yao.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa Daraja la Kigamboni na kuwataka wananchi kuhakikisha wanalitumia daraja hilo kwa usahihi na kuepuka vitendo vyote vya hujuma.

Amesema daraja hilo lililojengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 214 linatarajiwa kufunguliwa rasmi Aprili 16 na litakuwa na njia sita za magari na mbili za watembea kwa miguu.

"Nawataka wananchi na watumiaji wote wa daraja hili kuhakikisha kuwa miundombinu ya daraja haihujumiwi na watu wenye nia mbaya kwani vitendo vya aina hiyo licha ya kuharibu daraja vitahatarisha usalama wa watumiaji", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Naye Msimamizi wa Daraja hilo kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. Karim Mataka amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni umekamilika katika hatua zote na kinachosubitriwa na ufunguzi na kuanza kutumika.

Amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya daraja hilo kwa madereva na watembea kwa miguu ili kuepuka usumbufu siku za mwanzoni.

Daraja hilo litakalofunguliwa rasmi Aprili 16 litapunguza msongamano wa usafiri kwa wakazi wa kigamboni na maeneo ya katikati ya jiji la Dar es salaam.
Meneja wa mradi wa Ujenzi wa Flow Meter ya Kigamboni Eng. Mary Mhayaya akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi huo.
Muonekano wa Flow Meter mpya ya Kigamboni katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Muonekano wa Daraja la Kigamboni mara baada ya ujenzi wake kukamilika.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akijadiliana jambo na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni (kushoto) na Nahodha wa kivuko hicho (kulia) wakati alipokikagua.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipata maelekezo kwa Mkurugenzi Msaidizi Barabara za Mijini Eng. Hussein Mativila (kushoto) alipokagua Daraja la Kigamboni.