Thursday, April 14, 2016

TMAA yang’ara katika sekta ya madini



TMAA yang'ara katika sekta ya madini
Mtendaji Mkuu  wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini  Tanzania (TMAA), Dominic Rwekaza (pichani) akiwasilisha  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wakala huo kwa mwaka wa  fedha 2015/2015 mbele ya Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na watendaji wa Wizara  ya Nishati na Madini (hawapo pichani)
Mtendaji Mkuu  wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini  Tanzania (TMAA), Dominic Rwekaza (mbele) akiwasilisha  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wakala huo kwa mwaka wa  fedha 2015/2015 mbele ya Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na watendaji wa Wizara  ya Nishati na Madini.
Sehemu ya wajumbe  wa  Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na watendaji wa Wizara  ya Nishati na Madini wakifuatilia kwa makini  taarifa utekelezaji wa majukumu ya  Chuo cha Madini Dodoma (MRI) kwa mwaka wa fedha 2015/2016, iliyokuwa inawasilishwa na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Musa Magufuli (hayupo pichani)
Sehemu ya maofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini na  Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) wakifuatilia kwa makini  taarifa mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) Profesa Abdulkarim Mruma akisisitiza jambo katika kikao hicho.
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Kaimu Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi Ally Samaje (kulia) wakifuatilia kwa makini taarifa mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika kikao hicho.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Madini Dodoma (MRI) Musa Magufuli (pichani) akiwasilisha  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho kwa mwaka wa fedha 2015/2016, mbele ya  wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na watendaji wa Wizara  ya Nishati na Madini (hawapo pichani).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akifafanua jambo katika kikao hicho.

TMAA yang'ara katika sekta ya madini
Kamati ya Bunge yaipongeza
Yatakiwa kuongezewa fedha zaidi

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam 

Kamati ya  Kudumu ya Bunge  ya Nishati na Madini  hivi karibuni iliupongeza Wakala wa  Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA)  kwa  kazi nzuri ya kudhibiti madini yanayotoroshwa  nje ya nchini

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe wa kamati hiyo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wakala huo kwa kipindi cha  mwaka wa fedha 2015/2016, walisema kuwa wakala umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato katika sekta ya madini na kuitaka serikali kuuwezesha zaidi ili uweze kuzalisha zaidi na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kupitia sekta ya madini.

Mjumbe wa kamati hiyo, Suzan Kiwanga alisema kuwa TMAA ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi ya kudhibiti madini yanayotoroshwa nje ya nchi  kupitia  wataalam wake walioko migodini na  viwanja  vya ndege, hivyo ni vyema wakawezeshwa ili kufanya kazi hiyo  kwa bidii na uaminifu mkubwa.

"Kulingana na  ripoti yao, TMAA imefanya kazi kubwa ya kuokoa mabilioni ya shilingi  kupitia ukamataji wa madini yaliyokuwa yanatoroshwa nje ya nchi, kazi  waliyoifanya ni kubwa yenye kuhitaji  uaminifu mkubwa,  hivyo wakiwezeshwa zaidi wana uwezo wa kufanya vizuri zaidi," alisema Kiwanga

Naye mjumbe  mwingine wa kamati hiyo, Ikupa Alex aliongeza kuwa  wahalifu wanaokamatwa na TMAA wanatakiwa kufikishwa katika vyombo  vya sheria  na kutozwa faini kubwa  ili iwe  fundisho wa watoroshaji wengine.

" Huu  wakala ndio unaowezesha  Mamlaka  ya Mapato  Tanzania (TRA) kubaini kodi inayostahili kulipwa na makampuni yanayojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa madini nchini, rai yangu ni wakala huu kuwezeshwa zaidi katika nyanja zote ikiwamo  rasilimali fedha na  rasilimali watu ili uweze kufanya   kwa ufanisi zaidi," alisema Alex.

Awali  akielezea  mafanikio  ya  TMAA  tangu kuanzishwa kwake Mtendaji Mkuu  wa wakala huo, Dominic Rwekaza alisema  kwa kipindi cha  mwaka 2009 hadi Januari 2016, kampuni mbalimbali zimelipa jumla ya Shilingi bilioni 680.5 kama kodi ya mapato.


Aliongeza kuwa mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa malipo ya mrabaha kutokana na madini ya ujenzi na viwandani baada ya kufanyika kwa ukaguzi  ambao umewezesha  kiasi cha Shilingi bilioni 14 kulipwa kama mrabaha katika kipindi cha Juni 2011 hadi Januari 2016.

Alisema malipo hayo yametokana na uzalishaji wa jumla ya tani milioni 33.6 za madini ya ujenzi na viwandani yenye thamani ya Shilingi bilioni 465.7 kulingana na uhakiki uliofanywa na Wakala.

Aliendelea kueleza kuwa wakala  ulichangia kwa uongezeko  la malipo ya mrabaha kutokana na shughuli za uchenjuaji wa marudio kwa kutumia teknolojia ya vat leaching ambapo kiasi cha shilingi  bilioni 7.5 kililipwa  kama mrabaha katika kipindi cha Julai 2012 hadi Januari 2016.

Alifafanua kuwa malipo hayo yalitokana na uzalishaji na mauzo ya dhahabu kutoka kwa wazalishaji wanaotumia teknolojia ya "vat leaching" katika mikoa ya Mwanza, Geita na Mbeya ambapo kulikuwa na jumla ya kilo 3,046 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi bilioni 179.8 kulingana na uhakiki uliofanywa na Wakala.

Alisisitiza kuwa  wakala uliwezesha  serikali  kupata mrabaha na takwimu sahihi za madini yaliyozalishwa na migodi mikubwa nchinikupitia  ukaguzi na uhakiki madini yaliyozalishwa na kuuzwa na migodi mikubwa ya Biharamulo, Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, New Luika, North Mara, TanzaniteOne, Mwadui na Ngaka, ambapo ukaguzi huo ulisaidia kujua kiasi na thamani halisi ya madini yaliyozalishwa na kuuzwa.

"Ukaguzi huo umewezesha kukusanywa kwa jumla ya Dola za Marekani milioni 430 kama mrabaha kutoka kwenye migodi hiyo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2015," alisema  Rwekaza.

Akielezea udhibiti  wa utoroshwaji  wa madini kupitia  viwanja vya kimataifa vya ndege hapa nchini, Rwekaza alifafanua kuwa wakala  ulianzisha ukaguzi maalum wa kukagua madini yanayosafirishwa nje ya nchi kupitia Viwanja vya Ndege vya Julius Nyerere - Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza na kuwakamata watu wasio waaminifu wanaojaribu kusafirisha madini nje ya nchi kinyume cha sheria.

Alisema kupitia  ukaguzi huo  jumla ya matukio 89 ya utoroshaji wa madini yaliripotiwa hadi Desemba 2015 ambapo madini hayo yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 10.8 na Shilingi bilioni 1.1. na kuongeza kuwa wahusika wamechukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

Aliongeza kuwa  wakala  umekuwa ukifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa shughuli za ukarabati na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi mikubwa, ya kati na midogo ambapo wahusika wamekuwa wakipewa maelekezo yenye lengo la kuboresha hali ya mazingira kwenye maeneo yao.