Kampuni kutoka Falme za Kiarabu, Rental Solutions and Services LLC, imeiburuza mahakamani kampuni ya kufua umeme ya Symbion Tanzania Limited, ikidai kulipwa dola za Kimarekani 228,070,655.67, ambazo ni zaidi ya billion 560 za Kitanzania kama fidia na malipo ya ukodishaji wa mitambo ya kuzalishia umeme hapa nchini.
Kesi hiyo namba 234 ya mwaka 2016 imefunguliwa katika Mahakama Kuu Jijini Dar es Salaam mwisho mwa wiki iliyopita. Mdaiwa wa pili katika shauri hilo ni Shirika la Umeme, Tanesco, ambalo limeunganishwa katika kesi hiyo ya madai kama mdau mkuu kwenye sakata hilo ambapo maamuzi yatakayotolewa na mahakama yanaweza kuiathiri.
Katika hati ya madai, Kampuni ya Rental Solutions and services inadai Symbion dolla za kimarekani 28,070,655.67 kama malimbikizo ya gharama za ukodishwaji wa mitambo ambayo hadi sasa kampuni ya Symbion imeshindwa kulipa na pia katika shauri hilo Symbion itatakiwa kulipa dola za kimarekani million 200 ambazo ni fidia kwa kampuni hiyo kula hasara kutokana na Symbion kuvunja masharti ya mkataba na kuchelewesha au kushindwa kufanya malipo hayo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, fedha hizo zinatokana na kazi zilizofanywa na kampuni hiyo ya Uarabuni ya kusambaza, kusimika na kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ambayo ilikodishwa na Symbion kwa matumizi ya miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme kwa ajili ya Tanesco ili usambazwe kwenye gridi ya Taifa kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Rental Solutions and Services pia katika kesi hiyo inaiomba Mahakama kutamka kuwa kushindwa kwa Symbion kulipa gharama hizo za ukodishaji kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba na pande zote mbili kumepelekea uvunjifu wa mkataba na hivyo sio halali na haistahili kuendelea.
Inadaiwa kuwa kati ya Septemba 2011 hadi Juni 2013, Rental Solutions and services iliingia mikataba mbalimbali na Symbion ambapo pale ilipohijika mikataba hiyo iliongezewa muda ili kukidhi mahitaji kwa mujibu wa mikataba hiyo kwa lengo la kusambaza na kusimika mitambo ya umeme kwa aili ya kuasambazwa kwenye gridi ya Taifa.
Mnano September 21, 2011, kampuni hiyo ya Uarabuni iliingia mkataba na Symbion kwa aili ya kusambaza na kusimika mitambo ya umeme katika kituo cha Zuzu cha Tanesco chenye nguvu ya 33kv kilichoko Dodoma yenya uwezo wa kuzalisha Megawati 50.
Katika mitambo hiyo, pande husika zilikubaliana malipo ya dolla za Kimarekani 1,374,500 kwa mwezi kwa kipindi ambacho kingeishia miezi sita. Inadaiwa kuwa kwa kipndi hicho Symbion ingepaswa kulipa umla ya dola za Kimarekani 8,247,000.
Hati ya mdai inaonyesha kuwa mkataba kama huo uliingiwa na pande zote mbili Februari 12, 2012, kuhusiana na mitambo ya kuzalisha umeme wa Megawati 55 kwa kipindi cha miezi 12 kwa gharama ya dola za Kimarekani 1, 666, 000 kwa mwezi. Mitambo hiyo ipo katika vituo vya Arusha na Dodoma.
Kwa mujibu wa hati ya madai, kulikuwepo na ongezeko wa muda wa matumizi wa mitambo hiyo katika vituo vya Dodoma na Arusha ambapo Rental Solutions and Services ilitimiza matakwa yake kama ilivyo kwenye mikataba na kwamba iliwasilisha hati za malipo kwa Symbion kwa ajili ya kukamilisha malipo ya kukodi kitambo hiyo kama inavyotakiwa.
Pamoja na Rental solutions and Services kutimiza masharti ya mikataba hiyo, kati ya dola za kimarekani 77,667,666.28, Symbion imelipa kiasi cha dola za kimarekani 49,597,010.61 tu. Hivyo, Rental Solutions and Services inadai kuwa hadi sasa, bila uhalali wowote, Symbion imeshindwa kutimiza masharti ya mkataba kwa kutolipa kiasi cha dola za kimarekani 28,070,655.67.
Inaelezwa kuwa kushindwa kwa Symbion kulipa kiasi hicho cha fedha kimeisabishia Rental Solutions kula hasara kubwa kwa kushindwa kutumia kiasi hicho ambacho kilitakiwa kulipwa ndani ya muda uliokubaliwa.
Rental Solutions and Services inadai kwamba ilikuwa imeingia makubaliano na wadau wengine wa kukodisha mitambo hiyo iliyosambazwa kwenye vituo husika kwa ajili ya Symbion kwa ahadi kuwa Symbion ingelipa kiasi cha fedha kilichokubaliwa kwa wakati mara baada ya kulipwa na Tanesco.
Kati ya maombi ambayo Rental Solutions and Services imewasilisha mahakamani katika kesi hii ni kuamuriwa kwa Tanesco kukata fedha inayopaswa kulipwa Symbion na kuilipa Rental Solutions and Services moja kwa moja ili kufidia deni hilo.