Saturday, April 09, 2016

RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI, UKO MADARAKANI HADI SASA KWA USAFI UPI?



RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI, UKO MADARAKANI HADI SASA KWA USAFI UPI?
Jamal Malinzi, Rais wa TFF
Jamal Malinzi, Rais wa TFF

Na Martin M. M

Kuweka kumbukumbu sawa, TFF ni kifupi cha maneno, Tanzania Football Federation (shirikisho la mpira wa miguu Tanzania), baada ya hapo tunaweza kuanza kujadili hoja yetu.

Soka la nchi hii, limekumbwa na kashfa nzito sana ya upangaji wa matokeo katika michezo iliyokuwa ikihusisha vilabu vya ligi daraja la kwanza ngazi ya taifa.

Kashfa hiyo imelikumbuka shirikishola mchezo wa mpira wa miguu nchini (TFF), huku bado kukiwa na sintofahamu kubwa sana ya upangaji mbovu wa ratiba kwa kuzipendelea baadhi ya timu katika kuwania ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara..

Kamati ya nidhamu ya TFF, chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Wakili Jerome siku ya tarehe 3-04-2016, walilitolea uamuzi shauri la upangaji wa matokeo kwa mechi za Kundi C Ligi Daraja la Kwanza.

Kamati ya nidhamu ilipata fursa ya kuwahoji wakuu na viongozi wa vyama ngazi ya wilaya na mkoa ambapo timu husika zinatoka, walihojiwa ili kupata utimamu wa kashfa hiyo kabla ya kutoa maamuzi.

Klabu za Geita Gold Sport (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) zimekutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao.

Upande wa klabu ya JKT Kanembwa FC ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL), baada ya kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C.

Kamati ya Nidhamu imewafungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC vs Geita Gold, Saleh Mang'ola na kamisaa wa mchezo huo Moshi Juma baada ya kukutwa na hatia ya upangaji matokeo.

Aidha kamati pia imemkuta na hatia kocha msaidizi wa klabu ya Geita Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu.

Makipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Simba anayecheza kwa mkopo Geita Gold, wamefungiwa miaka 10 kutojihusisha na mpira wa miguu sambamba na kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kila mmoja.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Constantine Moradi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.

Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Yusuph Kitumbo, Katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Fateh Remtullah, Mwenyekiti wa klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian wamefungiwa maisha kutojihusisha na mpira wa miguu.

Mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi Tabora vs JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde wamefungiwa kwa muda wa miaka kumi kutojihusisha na mpira wa miguu, na kutozwa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kila mmoja.

Katibu wa klabu ya Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya Polisi Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia.

Nimeamua kuzitaja adhabu hizo ili kuweka kumbukumbu sawa, hali kama hii iliwahi kulikumbuka shirikisho la soka la nchi ya Italia 2006 pia nchi ya Ufaransa mwaka 1996.

Kashfa hiyo nchini Italia ilihusisha timu za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na zile za Daraja la Kwanza.

Timu zilizohusishwa na kashfa hiyo ni Juventus, AC Milan, Fiorentina, Lazio na Reggina baada ya mawasiliano ya simu kati ya viongozi wa timu hizo na waamuzi kunaswa wakati wakipanga mikakati ya kuhongana.

Juventus walikuwa mabingwa wakati huo ilituhumiwa kutoa rushwa ili kupangiwa waamuzi inaowataka. Kutokana na makosa hayo, klabu hiyo ilishushwa daraja huku Fiorentina na Lazio, AC Millan na Reggina zikipokwa pointi na kupigwa faini.

Ikumbukwe pia Mkurugenzi wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi, alifunguliwa mashtaka ya makosa ya jinai kwa makosa ya rushwa na baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka mitano na miezi minne jela.

Mmiliki wa Fiorentina, Diego Della Valle na Rais wa Lazio, Claudio Lotito walihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela na faini ya Euro 25,000 kila mmoja.

Mtendaji mkuu wa zamani wa AC Milan, Leonardo Meani alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.

Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Italia, Innocenzo Mazzini alihukumiwa kifungo cha miezi 26 jela wakati refa mstaafu Massimo De Santis alitupwa jela ya miezi 23 kutokana na ushiriki wao katika vitendo hivyo viovu.

Kashfa za watu kununua mechi zimewahi pia kuikumba Brazil mwaka 2005 baada ya refa Edilson Pereira de Carvalho kufungiwa maisha wakati refa Paulo Jose Danelon aliondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya nchi hiyo kutokana na kupokea rushwa ya kampuni za kamari ili kupanga matokeo ya mechi.

Mwaka 1994 soka la Ufaransa lilighubikwa na kashfa ya rushwa baada ya Rais wa klabu ya Olympique de Marseille, Bernard Tapie, kutuhumiwa kuhonga timu pinzani na matokeo yake timu yake ikashushwa daraja kutoka Ligi Kuu.

Marseille ilivuliwa ubingwa wa msimu wa 1992/93 wa Ligi Kuu ya Ufaransa na kupokwa haki ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, 'Super Cup' na Kombe la Klabu Bingwa za Dunia baada ya kuhusishwa na kashfa ya kununua mechi.

Ilibainika kuwa klabu hiyo iliwahonga wachezaji wa klabu ya Valenciennes FC, ambao walikuwa ni Jacques Glassmann, Jorge Burruchaga na Christophe Robert ili wacheze chini ya kiwango.

Nyota hao watatu walipigiwa simu na mchezaji wa Marseille, Jean-Jacques Eydelie, wakiahidiwa fedha ili wacheze chini ya kiwango na pia wahakikishe hawachezi rafu ili wachezaji wa Marseille wasiumie kwani walikuwa wanakabiliwa na mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1993 dhidi ya klabu ya AC Milan katika uwanja wa Olympiastadion jijini Munich, Germany.

Kutokana na kashfa hiyo ya rushwa, Tapie, ambaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya Ufaransa, alifungwa miaka miwili jela kwa kuhusika na makosa hayo.

Kwenye soka la Tanzania kumekuwepo na tuhuma na shutuma nyingi sana kuhusu matatizo ya rushwa mchezoni. Kati ya timu na timu kati ya wachezaji na wachezaji na pia kati ya viongozi wa timu hizo na wasimamizi wa michezo husika.

Kanuni za shirikisho la mpira wa miguu la kimataifa, halikubali na linapinga vitendo vya rushwa mchezoni kwa kiwango kikubwa sana hebu tutazame kanuni na taratibu za FIFA kuhusu rushwa zinasema nini;

Ibara ya 6 ya Kununi za Nidhamu za FIFA inaainisha hukumu ya makosa yanayotokana na watoa rushwa na upangaji matokeo kwenye soka.

Vifungu (a), (b) na (c) vya kanuni hizo vinaeleza kuwa mtu anayebainika kujihusisha na rushwa anaweza kuadhibiwa kwa kufungiwa maisha, kupigwa faini, au kutoruhusiwa kabisa kuingia katikia kiwanja chochote cha soka.

FIFA pia inaweza kuandaa utaratibu wa kufilisi mali za mtuhumiwa na mali zake kutumika kuendeleza soka ikiwa atahusishwa na masuala ya kutoa rushwa kwa marefa.

Ni wazi FIFA haikubali na haitoi mwanya kwa vitendo vya rushwa katika mchezo wa mpira wa miguu.

Ni nini maoni yangu kama mdau wa mchezo huu nchini?

Maoni yangu ni kama yafuatayo…

Kwa kuwa kamati tendaji ya TFF ipo na inaundwa na Rais wa shirikisho na ina mamlaka ya kujadili jambo lolote kubwa katika shirikisho, wapitie taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi daraja la kwanza, kuhusu upangaji matokeo uliziohusisha vilabu vya JKT Oljoro, Geita Gold Sport, JKT Kanembwa na Polisi Tabora na kisha baada ya hapo walipeleke suala hilo katika kamati ya nidhamu ya TFF (jambo ambalo tayari limekwisha kufanyika), baada ya hapo waitishe mkutano mkuu wa dharura katika kupitisha maamuzi ya kamati ya utendaji na baada ya hapo jambo hili lifikishwe kwenye ngazi za maamuzi ya kisheria katika nchi yaani TAKUKURU kwa sababu TFF hawana mwanya na meno ya kuweza kushtaki kwa makosa ya jinai ila ya kimichezo tu.

Kwa sababu sakata hili limegusa pia baadhi ya watendaji wa idara mbalimbali za serikali, ni muhimu wahusika wakatajwa, wakachukuliwa hatua za kisheria kwa kutumia ofisi za umma kwa maslahi yao binafsi.

Pia, TFF iendelee na uchunguzi yakinifu, kuwabaini watu waliohusika na kuratibu mchezo huu mchafu tangu mwanzo na pia ambao wanamiliki tabia hizi za upangaji wa matokeo ili kutoa adhabu kali za kimichezo na pia kuwafikisha kwenye taasisi za kuzuia na kupambana na Rushwa.

Kuna baadhi ya wachezaji ndiyo vinara wa kashfa za kupanga matokeo. Wanatumika sana kuharibu mchezo huu washaghuliliwe ipasavyo.

Rais wa shirikisho la soka la Tanzania (TFF), Jamal Malinzi pia hadi sasa amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa shirikisho hilo kwa sababu kwenye uongozi wake kumeibuka kashfa mbalimbali na maendeleo ya mpira yamezidi kushuka chini kwa kasi. Malinzi anapaswa kujipima kama kweli anatosha kuendelea kuongoza mpira wa nchi hii kwa kashfa hizi na namna soka linsvyokwenda.

TFF imepoteza mwelekeo

TFF chini ya Malinzi wameshindwa hata kukomboa mzigo wa nyasi bandia kutoka bandari ya DSM kwa kisingizio hawana fedha za ushuru. TFF juzi wamekamatiwa magari yao na TRA kisa wanadaiwa ushuru wa zaidi ya bilioni 3 hivi kweli kuna kitu katika mpira kitaendelea chini ya Jamal Malinzi?

Kashfa za upangaji matokeo, kashfa ya urudufu wa ratiba katika kuzipendelea timu kadhaa katika ligi kuu, kashfa ya kushindwa kuliendesha shirikisho na kudaiwa madeni mengi, kashfa ya kuwa na ubia na timu inayoshiriki ligi daraja la pili (Alliance) ya jijini mwanza na kuhusika katika kununua mechi kadhaa, ZINATOSHA KUMPA TAA NYEKUNDU JAMAL MALINZI.

(Makala imeandikwa kwa kutumia vyanzo na machapisho mbalimbali ya habari)

Martin Maranja Masese,
Mwananchi wa kawaida,
+255719715520
martinchizzle@gmail.com