Thursday, April 07, 2016

Muogeleaji Sonia Tumiotto ashinda medali ya dhahabu Dubai





Muogeleaji Sonia Tumiotto ashinda medali ya dhahabu Dubai
Muogeleaji nyota wa Tanzania, Sonia Tumiotto ameshinda medali ya dhahabu katika mashindano ya kimataia ya Dubai yajulikanao kwa jina la Dubai International Aquatics Championships.

Sonia alishinda medali ya dhahabu katika staili ya backstroke kwa waogeleaji wenye umri kati ya miaka 14 na 15 na kuweka rekodi ya kushinda medali mbili katika mashindano hayo ambayo pia yanatumika kutafuta waogeleaji wa kufuzu mashindano ya Olimpiki.

Awali Sonia alishinda medali ya shaba katika staili ya freestyle mita 400 kwa kutumia muda wa 4.49.40 ambapo katika staili ya backstroke, alitumia muda wa sekunde  32.77 katika mita 50.  hata jivyo, pamoja na kushinda, muogeleaji huyo hajatapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Olimpiki kutokana na taarifa za Fina kuwa imeondoa mashindano yote ya 'stroke' kwa mita 50 na ya kupokezana maarufu kwa jina la 'relay'.

Ushindi huo umepokelewa kwa furaha na katibu mkuu wa klabu ya Dar Swim Club (DSC), Inviolata Itatiro kwa kusema kuwa wamefarijika na wanaamini kuwa Tanzania inaweza kufanya vyema katika mashindano hayo ya kimataifa endapo changamoto mbalimbali za mchezo huo zitatatuliwa.

 "Sonia ni zao la DSC na kwa sasa anaiwakilisha nchi katika kutafuta tiketi za kufuzu katika mashindano ya Olimpiki, ni faraja kubwa kutokana na ukweli kuwa amethubutu kuonyesha kuwa tatizo ni  vifaa bora vya mchezo huo na mazoezi," alisema Inviolata.

Alisema kuwa Sonia kwa sasa anasoma shule nchini Uingereza ambapo anafanya mazoezi kwa kutumia vifaa bora na muda mwingi tofauti na hapa nyumbani kuwa hatuna vifaa hivyo pamoja na bwawa la mita 50 la kuogelea.

"Muda wa mazoezi ni mfupi kulinganisha na wenzetu, hii inatokana na gharama kubwa za kukodi bwawa la kuogelea, kuna vilabu vinalipa sh40,000 kwa saa, hivyo ukifanya mazoezi kwa msaa manne, utalipa hele nyingi zaidi, kama kungekuwa na bwawa la jumuiya, nadhani waogeleaji wetu wangefanya mazoezi muda mrefu na kuwa na wastani mzuri katika mashindano," alisema.

Inviolata anaamini kuwa Sonia na waogeleaji wengine, Hilal Hilal, Collins Saliboko na Aliasghar Karimjee bado wana nafasi ya kupata muda wa kufuzu katika mashindano ya Olimpiki katika mashindano hayo ambayo yanamalizika leo.