Thursday, April 14, 2016

Miss Tabata 2016 kuanza mazoezi Jumanne



Miss Tabata 2016 kuanza mazoezi Jumanne
Miss Tabata 2014 Ambasia Mallya
MAANDALIZI ya kumsaka mrembo wa kitongoji cha Tabata mwaka huu 'Miss Tabata 2016' yanatarajiwa kufanyika kuanzia Jumanne Aprili 19 kwenye Ukumbi wa Da West Park, Tabata jijini Dar es Salaam.
 
Mratibu wa shindano hilo Joseph Kapinga alisema jana kuwa warembo wote waliojiandikisha wanatakiwa kufika mazoezini na bado fomu za kushiriki shindano hilo zinaendelea kutolewa.
 
Kapinga alisema kwamba Keen Arts ambayo ni kampuni tanzu ya Bob Entertainment ndiyo imepewa kibali cha kuendesha shindano hilo na waratibu wa taifa Lino Agency iliyoko chini ya mkurugenzi wake Hashim Lundenga.Mratibu huyo alisema uzinduzi rasmi wa shindano hilo utafanyika mwishoni mwa mwezi huu.
 
"Baada ya uzinduzi washiriki watatembelea hifadhi ya Mikumi na Dar es Salaam Zoo ikiwa ni njia mojawapo ya kutangaza utalii wa ndani," Kapinga alisema.Aliwataka warembo wenye sifa za kushiriki shindano hilo kujitokeza na kusema fomu hizo pia zinapatikana kwenye ukumbi wa Da West Park na ofisi za Miss Tanzania zilizoko Mikocheni.
 
Miss Tabata ni miongoni mwa vituo vitatu vilizoko kanda ya Ilala huku vingine vikiwa ni Ukonga na Dar City Centre.Washiriki watano kutoka kila kituo watashiriki kwenye shindano la Miss Ilala na hatimaye Miss Tanzania baadaye mwaka huu.
 
Ambasia Mallya ndiye mrembo anayeshikilia taji la kitongoji hicho ambacho kimetoa wawakilishi waliofanya vizuri katika ngazi ya taifa.Wadhamini ambao wameshathibitisha kudhamini shindano hilo ni pamoja na CXC Africa, Fredito Entertainment, Saluti5 na Bob Entertainment.