Tuesday, April 12, 2016

MFUMO FUNGANISHI WA KIELEKTRONIKI KWA AJILI YA USIMAMIZI WA SEKTA YA ARDHI WATAMBULISHWA KWA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII



MFUMO FUNGANISHI WA KIELEKTRONIKI KWA AJILI YA USIMAMIZI WA SEKTA YA ARDHI WATAMBULISHWA KWA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII
Mratibu wa Programu ya mfumo funganishi wa kielekroniki kwa ajili ya usimamizi wa sekta ya ardhi (Integrated Land Information System /ILMIS) Barney Laseko ametambulisha Mfumo huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii – Dar es Salaam wakati wa uwasilishaji wa utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Ardhi kwa mwaka 2015/2016 kwa kamati hiyo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu ILMIS, Bwn. Laseko alisema mfumo una lengo la kuondoa changamoto za upatikanaji na utunzaji wa taarifa ili kuongeza tija kwa kupunguza muda na gharama za huduma za Ardhi kwa Wananchi.

Alitaja kazi zitakazofanyika sambamba na uanzishwaji wa ILMIS ni pamoja na; Kuandaa kumbukumbu zote za zamani ili ziweze kuingizwa kwenye kompua (digization), Ujenzi wa kituo maalum cha kuhifadhi Kumbukumbu, Kusimamia, Kufundishia, Kutatua matatizo na kuhakiki mawasiliano ya Kanda, Mikoa, Halmashauri na Watumiaji wengine wa ILMIS, Uhamishaji wa Kumbukumbu za zamani na Upigaji wa picha za Anga (Base Map), ambao kutokana na ukubwa wa nchi wa kilomita za mraba 947,000, pesa zitakazohitajika ni kati ya US$ 26.3 Milioni hadi US$ 189.4 Milioni katika eneo hilo la upigaji picha.

Aidha, Bwn. Laseko alisema matokeo ya ufanyaji kazi kwa mfumo huo yatakuwa na faida zifuatazo; Taarifa zitapatikana kwa njia ya satellite kwa uhakika zaidi, Taarifa zote za kwenye mafaili na karatasi zilizozagaa zitahifadhiwa kielectroniki Makao Makuu, Ofisi za Kanda na sehemu maalum. Vile vile kazi zote za kuchora na kutumia taarifa zitafanywa kwa kompyuta.

ILMIS inaendelea na mchakato wa ujengwaji wake kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mratibu wa Programu ya mfumo funganishi wa kielekroniki kwa ajili ya usimamizi wa sekta ya ardhi (Integrated Land Information System /ILMIS) Barney Laseko akitoa taarifa fupi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mfumo huo kwa kamati ya ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii – Dar es Salaam.
Baadhi ya vifaa vya upimaji vya kisasa vinavyoendana na mfumo mpya wa upimaji/ Digital equipment, vitakavyotumika sambamba na mfumo wa funganishi wa kielekroniki kwa ajili ya usimamizi wa sekta ya ardhi.