Sunday, April 03, 2016

Kampuni ya Kimataifa ya hesabu PKF International yaungana na KLSA Associates ya Dar es salaam



Kampuni ya Kimataifa ya hesabu PKF International yaungana na KLSA Associates ya Dar es salaam
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad, amezitaka kampuni za ukaguzi wa hesabu nchini kufanyakazi zao kwa weledi na kujiepusha na hadaa ili kuwezesha serikali, mashirika na kampuni  lengwa kutumiza malengo yao ipasavyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano baina ya kampuni ya Kimataifa ya PFK na KLSA Associates ya jijini Dar es Salaam jana, Profesa Assad alisema nidhamu ya matumizi ya pesa itaweza kwenda vizuri iwapo tu wakaguzi watakuwa waadilifu na wenye mapenzi na kazi yao.
Alisema kuna kampuni mojawapo nchini iliwahi kupewa kazi ya ukaguzi wa hesabu za serikali lakini kilichokuja kutokea ni tofauti na matarajio jambo ambalo hatarajii litokee tena kwa sasa na amewataka wamiliki wa makampuni hayo kujali na kuthamini mafunzo.
Alisema mafunzo kwa wafanyakazi ni muhimu ili kuwajengea uwezo wao kiutendaji na kuwafanya wawe na ufahamu mpana katika taaluma yao na upande mwingine amewataka watanzania kubadilika sasa na kuachana na mfumo uliopitwa na wakati wa kutaka kulipwa hata wanapofundishwa.
 "Kuna wafanyakazi ingawa mafunzo kwa ajili yake na yangemfanya awe bora zaidi lakini cha ajabu kuna ambao kama wakielezwa kuwa hakutakuwa na posho au malipo mengine yanayofanana na hayo hawaonekani" alisema.
Awali akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushrikiano huo, Msimamizi wa Ushirikiano wa PKF Associates  Tanzania ambao wamebadili jina kutoka la awali la KLSA Associates baada ya muungano huo, Mustansir Gulamhussein alisema ndoto ya muda mrefu ya kampuni hiyo imetimia.
Alisema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi na sekta karibu zote muhimu kama zilivyo zingine zinahitaji ukaguzi na utunzaji wa hesabu, kodi na ushauri wa kibiashara na wamejipanga kuhakikisha wanatioa huduma tarajiwa.
Alisema kampuni yake kabla ya ushirikiano huo na PKF ilijikita katika ukaguzi na ushauri wa kitalaam wa masuala ya utunzaji wa hesabu na ukaguzi katika masuala ya kilimo, fedha, nishati, utalii, mawasiliano, uhandisi na huduma za serikali.
Katika hatua nyingine PKF ilitoa msaada wa dola za Marekani 4000 (TSh. Milioni 8 na ushee) kwa ajili ya shule za msingi za Koma na Kuruti zilizopo visiwa vya mkoa wa Pwani na taa za umemejua 40 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya bweni ya Kisiju. 
 Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad (kulia), akimkabidhi cheti cha utambuzi wa ushirikiano kutoka kwa Msimamizi wa Ushirikiano wa Kampuni ya PKF Associates, Mustansir Gulamhussein katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam jana.
 Watendaji wakuu wa kampuni ya PKF, wakifuatilia hotuba ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad (kulia), wakati wa uzinduzi huo.
 Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad (kulia), akizungunmza wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Kampuni ya PKF Associates, Bw. Theo Vermaak akizungunza wakati wa hafla hiyo.