Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mali Asili linakusudia kuongeza mashirikiano na kuwasaidia wananchi wanaoanzisha vitalu vya mikarafuu Unguja na Pemba.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bibi Mwanahija Almasi ametoa ahadi hiyo baada ya ziara yake ya siku mbili kutembelea vitalu vya mikarafuu vya Serikali na vya watu binafsi katika vijiji vya Kitope, Kidimni, Machui Selem na Donge kuona matatizo yanayowakabili katika kutekeleza kazi zao.
Amesema vitalu vya watu binafsi vinamchango mkubwa katika kuimarisha zao la karafu Zanzibar kwa kuziba pengo linalojitokeza wakati wa ugawaji wa miche ya mikarafuu kwa wakulima kutoka vitalu vya Serikali
Amesisitiza kuwa kutoakana umuhimu huo na kazi kubwa wanayochukua wakulima hao huku wakikabiliwa na upungufu wa nyenzo muhimu, Shirika litatoa pembejeo zitakazosaidia kufanikisha kazi zao kwa ufanisi.
Wakati wa ziara hiyo wakulima wanaomiliki vitalu vya mikarafuu walimueleza Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC kwamba wanakabiliwa na tatizo la vifuko vya kuatikia miche (policing), mabero, pauro na maji hasa wakati wa kiangazi.
Mkurugenzi Mwendeshaji amewataka wakulima hao kutovunjika moyo na changamoto wanazokabiliana nazo na waendelee kushirikiana na maafisa wa Kilimo wakati Shirika linafanya juhudi za kupunguza changamoto zao.
Hata hivyo Bi Mwanahija amewashauri wenye vitalu vya mikarafuu baada ya kupata msaada kutoka ZSTC kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya kuuzia miche ya mikarafuu kwa wakulima ambapo hivi sasa wanauza shilingi 1000 kwa mche mmoja.
Amesema Serikali itaendelea kutoa miche ya mikarafuu bure kwa wakulima lakini vitalu vya Serikali viliopo hivi sasa haviwezi kukidhi mahitaji ya wakulima wote wa zao hilo, hivyo vitalu vya watu binafsi vitaendelea kuwa tegemeo kwa wakulima
"Wakulima wa vitalu vya Mikarafuu mumekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza na kuimarisha zao la karafuu Zanzibar lakini wapunguzieni wakulima bei ya miche ingawa gharama mnazotumia ni kubwa," Bi Mwanahija aliwashauri.
Bibi Mwanahija amewaelekeza maafisa Kilimo kuwapa wakulima miche ya mikarafuu wanayoweza kuihudumia kwani uzoefu unaonyesha wakulima huchukua miche mingi wasiyoweza kuitunza na hatimae inakufa mara tu baada ya kumaliza mvua za masika.
Mkuu wa Vitalu kutoka Wizara ya Kilimo Rashid Nassor Rashid alimueleza Mkurugenzi Muendeshaji wa ZSTC kwamba vitalu vya Serikali vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi baada ya wengine kustaafu na baadhi yao kuzeeka hivyo wanampango wa kuajiri wafanyakazi wa muda kwa kazi za dharura kuziba pengo liliopo.
Amesema kazi ya kutafuta mbegu (matende) kwa ajili ya vitalu vya mikarafuu zinachukua muda mfupi kabla ya mvua za masika kuanza na ikiwa kazi hiyo haitofanywa kipindi cha sasa kazi hiyo itashindwa kutekelezwa.
Mkuu wa usimamizi wa zao la Karafuu kutoka Wizara ya Kilimo na Mali Asili Badru Kombo Mwemvura amemuhakikishia Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC kwamba iwapo wakulima watafuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo lengo la Serikali la kuongeza uzalishaji wa Karafuu litafika muda mfupi ujao.
Amesema tatizo la wakulima wa zao la karafu ni kuchukua miche mingi bila ya kuwa na uwezo wa kuihudumia na baadhi yao huchelewa kuipanda baada ya kuchukua hatimae hufa huku wengine wakikosa kabisa.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakiathiri sana nchi za visiwa nayo imekuwa changamoto kubwa kwa kilimo cha zao la Karafuu na mazao mengine Zanzibar.
Wizara ya Kilimo ilipanga kutoa miche ya Mikarafuu milioni moja kwa wakulima wa zao hilo Unguja na Pemba, kuanzia mwezi wa April, lakini kutokana na ukosefu wa mbegu ulijiotokeza mwaka jana kiwango hicho huenda kikapungua
Mkulima wa vitalu vya karafuu wa Kitope Mzee Sheha Khamis a akisikiliza baada ya kumuelezea Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ZSTC changamoto anazokabiliana nazo katika kutekeleza kazi hiyo wakati Mkurugenzi huyo alipofanya ziara katika Mkoa Kaskazini Unguja na Wilaya Kati.
Kitalu cha Mikarafuu cha Serikali cha Donge Mwanakombo kikionekana kikiwa na miche ya kutosha ikiwa tayari kupewa wakulima wa zao hilo wakati wa mvua za masika zitakapoanza mwezi ujao.
Mfanyakazi wa kitalu cha Mikarafuu cha Donge Bi Fatma akitayarisha udongo kwa ajili ya kuatika miche katika shamba hilo linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo na Mali Asili.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bibi Mwanahija Almasi akizungumza na waandishi wa habari katika kitalu cha S erikali cha Kivunge baada ya kumaliza ziara ya siku mbili kutembelea vitalu vya mikarafuu vya Mkoa Kaskazini AUnguja na Wilaya ya Kati. PICHA NA RAMADHANI ALI/HABARI MAELEZO ZANZIBAR.