Thursday, March 17, 2016

Waziri Nape awataka wauzaji wa Filamu za Nje kufuata sheria



Waziri Nape awataka wauzaji wa Filamu za Nje kufuata sheria
Na Shamimu Nyaki

Kufuatia kuwepo kwa Filamu nyingi za nje zinazouzwa hapa nchini bila kufuata Sheria ya uuzaji wa kazi hizo Serikali imewataka wauzaji hao kufanya biashara hiyo kwa kufuata na kuzingatia sheria iliyowekwa ili kusaidia kukuza na kutangaza filamu za hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye wakati alipokuwa akizungumza na wauzaji wa Filamu hizo leo jijini Dar es Salaam.

Amewataka wauzaji hao kuwa na mkataba pamoja wamiiki wa kazi hizo ili waweze kufanya biashara hiyo kwa uhalali kwakua Serikali itawasaidia kusimamia utekelezaji wa mikataba hiyo na kurahisisha utekelezaji wa sheria iliyopo.

"Lazima mfuate na kutekeleza Sheria iliyopo kwakua mimi nipo hapa kuisimamia na kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa".Alisema Mhe.Waziri Nape.

Aidha katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo ameongeza kuwa ni lazima wauzaji wa filamu hizo kuhakikisha kuwa filamu wanazouza zimehakikiwa na bodi ya filamu pamoja na COSOTA ili kudhihirisha ubora wa kazi hizo na viwango vya hapa nchini.

"Ni lazima muhakikishe kazi mnazouza zimeruhusiwa na Bodi ya filamu pamoja na COSOTA na zinafuata madili ya hapa nchini''.Aliongeza Bi. Joyce.

Ameongeza kuwa bodi ya Filamu pamoja na COSOTA wapo tayari kuwasaidia kupata haki miliki ya filamu hizo wanazouza kwa kuwa wao ndio wenye dhamana ya kuruhusu filamu gani inastahili kuuzwa na ipi haistahili kuwepo sokoni.

Uuzaji wa filamu za nje hapa nchini umechangia kwa kiasi kikubwa filamu za hapa nchini kukosa soko hali inayochangia kudidimia kwa sanaa hiyo hapa nchini ambayo inatoa ajira nyingi kwa vijana.
Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akizungumza na wauzaji wa filamu za nje kuhusu kufuata sheria ya uuzaji wa filamu hizo hapa nchini katika kikao kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bi.Joyce Fissoo.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo akieleza jambo wakati kikao kati ya Serikali na wauzaji wa Filamu za nje(Hawapo Pichani) kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam .Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Bodi hiyo Bw Tairo.
Mwenyekiti wa wauzaji wa filamu za nje Bw Joseph Lyakurwa akiwasilishwa mada kwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye wakati wa kikao baina ya Serikali na wauzaji wa filamu hizo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wauzaji wa Filamu za nje walioshiriki katika kikao kati yao na Serikali cha kubadilisha sheria ya uuzaji wa filamu za nje hapa nchini kilichofanyika leo jijjini Dar es Salaam. Picha na Shamimu Nyaki.