Mhe. JPM awali ya yote napenda kukupongeza kwa kwa kazi nzuri ya kusafisha uchafu ndani ya nchi almaarufu kutumbua majipu. Kero za wananchi zipo katika ngazi mbalimbali na wewe mwenyewe ulizianisha kwa kina katika kampeni zako wakati ukitafuta nafasi ya kuliogoza taifa hili. Wakati wewe umekuwa muwazi katika kuondoa kero kwa wananchi, nichelee kusema watendaji wengi wa serikali za mitaa (sio wote) maisha yao yamekuwa yakineemeka kwa kuongeza kero kwa wananchi, hasa wa kipato cha chini.
Wamekuwa wakiongeza kero kwa wananchi wanyonge ili waendelee kuwanyonya kwa kwa njia moja au nyingine. Hili kwa kiwango kikubwa liko kwenye Serikali za mitaa na mabaraza ya ushauri ya kata, mengi yao ni kero kubwa sana na yanalalamikiwa na wananchi wazi wazi au chini chini kwa kuogopa manyanyaso kutoka kwa wakubwa hao.
Ingawa nafasi nyingi za uongozi katika ngazi hizo ni za kujitolea watu wamefanya kazi hizo ni za kudumu(full time) kwa ajili ya kujineemesha. Watu wanyonge wasio na kitu wengi wao hawapati haki kabisa au zinacheleweshwa. Kwani hili shauri lako lisikilizwe na wajumbe waje kwenye eneo la tukio kwa ajili ya ushauri lazima ulipe posho za wajumbe? Wajumbe wa mabaraza ya kata na mitaa wamekuwa Miungu watu.
Baadhi ya wajumbe wa mabaraza ya mitaa na kata wamekuwa watendaji wa kudumu na wanashinda katika ofisi hizo siku nzima wakifanya ndio eneo lao la ajira la kupatia kipato, na kutumia mbinu mbali mbali ambazo zinaongeza kero kwa wananchi wanyonge(hilo liko zaidi kwenye mitaa na vitongoji vya mijini). Nashukukuru Waziri Simbachawene alilwahi kuzungumzia hili katika ziara yake mkoani Morogoro.
Ngoja nitoe mifano michache; Hivi karibuni nimeshuhudia watu wawili wameziba kwa ukuta njia ya kwenda kwenye makaburi ya waislamu katika mtaa wa Boko Dovya, eneo la Somji Dar es salaam, serikali ya mtaa inafahamu, serikali ya kata inafahamu, lakini kwa kuzibwa midomo kwa njia ambazo hazieleweki, wanyonge wamenyimwa haki yao ya kutumia njia ya kwenda makaburini kwa miaka zaidi ya mitatu hivi. Mpaka sasa walioziba njia hiyo ambao kati yao ni wafanyakazi wa serikali ya JPM bado wameendelea kuwa na kiburi na kupingana kwa vitendo na nia ya dhati ya serikali ya JPM ya kuwaondolea wananchi wanyonge kero.
Siku moja nilitembelea ofisi ya mtaa mmoja nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Nilishtushwa na maneno ya baadhi ya wajumbe katika ofisi ile. Kulikuwa na mwananchi mmoja alikuwa anakuja kwa mbali kuja kupata huduma katika ofisi hiyo, wajumbe wakamuona, na wakaanza kuambiana angalia yule jamaa anakuja, hana hela achana naye. Nilishtuka sana, na kujiuliza hawa ndio wawakilishi wa wananchi au wachuuzi katika ofisi ya serikali? Lakini Nikaa kimya, baada ya muda nikaanzisha mazungumzo kuhusu serikali ya JPM na utumbuaji majipu, mjumbe mmoja mwanamama akanishangaza tena kwa maneno yake, akasema majipu wanatumbua huko juu huku chini hawawezi kutufikia tutaendelea kula tu.
Baada ya kusikia maneno hayo nikaishiwa nguvu na kujiambia mwenyewe kuwa serikali ya JPM ina kazi kwelikweli. Lakini Mhe. JPM napenda kukuhakikishia kuwa tupo nyuma yako, kuna watu wako tayari kufanya kazi na wewe iwe jua au mvua, ili mradi Tanzania irudi kwenye mstari na wananchi wanyonge wapate haki zao. Tunawaomba wakuu wa wilaya watembelee kata zote katika wilaya zao waongee na wananchi na ikiwezekana wawe na simu ofisini kwao kwa ajili kupokea ujumbe wa kero za wananchi, wananchi wapewe namba ya simu hiyo. Mkuu wa wilaya awe anapata majumiisho ya kero za wananchi kila siku/au kila wiki na kuzitolea maagizo/maamuzi. Maafisa tarafa kwa sehemu za vijijini nao wawe na utaratibu wa kupokea taarifa za wananchi na kuzifanyia kazi kwa niaba ya mkuu wa wilaya.
Serikali za mitaa na vitongoji ambazo zitaonekana zinalalamikiwa sana na wananchi basi mtendaji hasimamishwe kazi na serikali ya mtaa ivunjwe kwa kufuata taratibu , sheria na mamlaka aliyopewa waziri mwenye dhamana. Mtendaji wa kata na afisa tarafa wawajibike kwa kushindwa kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.
Wananchi wamechoshwa na kero ambazo zinasababishwa na viongozi serikali za mitaa na vitongoji ambao wengi wao wamegeuza matatizo ya wananchi kuwa miradi yao ya kujineemesha. Ni vyema utumbuaji majibu unaoendelea katika ngazi za juu uende sambamba na utumbuaji majibu katika ngazi za serikali ya mitaa na vitongoji ambako watanzania wengi ndiko waliko.
Mungu ibariki Tanzania
Mdau