Tuesday, December 15, 2015

TAFFA YAIBUA MAPYA YA UTOROSHAJI WA KONTENA


TAFFA YAIBUA MAPYA YA UTOROSHAJI WA KONTENA

Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), Stephen Ngatunga (kulia), akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na njia zinazotumika kuiba mapato ya serikali bandarini na katika Idara ya Forodha, Jijini Dar es Salaam jana. kushoto ni maofisa waandamizi wa chama hicho. Picha na Mpigapicha Wetu

Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), Stephen Ngatunga (kushoto), akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na njia zinazotumika kuiba mapato ya serikali bandarini na katika Idara ya Forodha, Jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Ofisa Mwandamizi wa chama hicho, Ernest Kallaghe.


Chalila Kibuda, Globu ya Jamii 
CHAMA cha Mawakala wa Forodha nchini (TAFFA) kimesema kuwa wizi wa kontena bandari ya Dar es Salaam na kusababisha serikali kukosa mapato ni tatizo la muda mrefu ambalo ni limekuwa likisababishwa na watumishi wa bandari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Rais wa TAFFA, Steven Ngatunga amesema tatizo lilojitokeza ya uondoshaji wa kontena 329 katika bandari Kavu ya Azam ilitokana na baadhi ya watumishi wa baadhi ya benki na Bandari kuingilia taarifa katika mfumo na kusababisha serikali kukosa mapato. 

Ngatunga amesema kuwa tatizo la serikali kukosa mapato katika bandari ya Dar es Salaam walishagundua lakini serikali ilishindwa kuchukua hatua mpaka serikali ya awamu ya tano kugundua hilo na hatua zimechukuliwa kwa wale waliohusika.

Amesema TAFFA itatoa ushirikiano kwa kile ambacho wanakiona katika bandari ya Dar es Salaam juu ya watu wanaosababisha serikali kukosa mapato kwa maslahi yao binafsi.

Aidha amesema kuwa kuna kampuni zilionekana kuwa zipo kwa ajili ya kukwepa kodi ya serikali ambazo chama kiliona na kupeleka malalamiko ambayo mwisho wa siku kukawepo urasimu wa kukutana viongozi ambao wanaweza kushughilikia hilo.

Amesema baadhi ya mawakala walilipia kontena lakini wanaambiwa malipo hayakufanyika huku wakiwa na kumbukumbu za malipo na kusababisha kutilia shaka juu ya uadilifu wa watumishi wa benki pamoja na bandari.

TAFFA imesema haiko tayari kwenda na mawakala ambao wanaharibu taaluma hiyo na kusababishia serikali kukosa mapato ambayo ndio ya kufanyia maendeleo nchini.

Amesema kuwa kuna kampuni 73 zimefungwa wakati hawahusiki katika katika uondoshaji wa kontena katika bandari na bandari kavu kutokana na kampuni hizo kuwa kulipia kontena zinazodaiwa kukwepa kodi.