Saturday, December 19, 2015

Rais Magufuli amtumia salamu za Rambirambi Rais Kikwete kwa kufiwa na Dada yake



Rais Magufuli amtumia salamu za Rambirambi Rais Kikwete kwa kufiwa na Dada yake


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amepatwa na msiba mzito wa kufiwa na Dada yake Mpendwa Bi. Tausi Khalfan Kikwete kilichotokea jana tarehe 17 Desemba, 2015 huko nchini India.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema anaungana na familia ya Rais Mstaafu Kikwete katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mtu muhimu kwa familia."Kwa masikitiko makubwa nakupa pole nyingi Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kufiwa na dada yako ambaye alikua nguzo muhimu katika familia" Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amemuomba Rais Mstaafu Kikwete kumfikishia salamu nyingi za pole kwa familia nzima na amewaomba wawe na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.Rais Magufuli amemuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aipumzishe roho ya marehemu Tausi Khalfan Kikwete mahali pema peponi, Amina.

Imetolewa na;
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU


18 Desemba, 2015