Thursday, December 03, 2015

DAWASCO YATANGAZA KUANZA KUTUMIKA KWA BEI MPYA YA MAJI JIJINI DAR



DAWASCO YATANGAZA KUANZA KUTUMIKA KWA BEI MPYA YA MAJI JIJINI DAR
Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam,(DAWASCO), limeanza rasmi kutumia bei zake mpya za ankara ya Maji, ikiwa ni siku chache tu baada  ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma ya  Nishati na Maji (EWURA) kupitisha  mapendekezo ya kupandisha gharama hizo zilizotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ili kusaidia kuboresha  huduma ya Majisafi na salama jijini Dar es salaam, Kibaha, na Bagamoyo mkoani Pwani.

Gharama hizo mpya ambazo zimeanza rasmi kutumika Disemba 01, zimepanda kutoka kiasi cha shilingi 1098 kwa unit 1 ya ujazo wa Maji ambayo ni sawa na lita 1000, hadi kufikia shilingi 1663  ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 51%. 

Ilielezwa kuwa Kupitishwa kwa mapendekezo hayo kutaongeza uwezo wa DAWASCO kufanya maboresho ya huduma za Maji na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wateja na kuwafanya wateja hao kuwa na uhakika wa huduma hiyo kwa kukamilisha miradi mbalimbali mikubwa ya Maji ambayo tayari ipo katika hatua zake za mwisho.

Wakizungumzia gharama hizo mpya za Maji wakazi wa jijini  Dar es salaam, wametoa maoni yao kuhusu ongezeko hilo jipya la bei za maji, ambapo wengi wao wameonesha kuridhika na bei hiyo mpya lakini wameiomba Dawasco kuhakikisha inawapatia huduma hiyo kulingana na mahitaji yao huku ikiendana na gharama iliyoongezwa. 

"Sisi hatuna shida kabisa na hiyo bei, tunachotaka ni maji, Dawasco wahakikishe wananchi tunapata huduma hiyo bila usumbufu wowote, sio mnaongeza bei halafu maji yenyewe hatupati, hapo hatutakubali kabisa" alisema Bi. Penieli Tenga mkazi wa Mwananyamala.

Mkazi mwingine wa Kinondoni Bi. Agness Mbwana ameonesha kuridhika na gharama hizo japokuwa hapo awali hakuwa na taarifa za ongezeko hilo la maji, mkazi huyo ameiomba Dawasco kutoa taarifa mapema ili wanapopata bili zao wasishangazwe na kiasi cha bili kilicholetwa.

Kwa upande wa DAWASCO, Kaimu Meneja Uhusiano Bi Everlasting Lyaro alisema bei hiyo mpya imeanza kutumika rasmi desemba mosi na wanaendelea kuwaelimisha wananchi wa maeneo mbalimbali juu ya ongezeko hilo ili kuepuka usumbufu wakati wa ulipaji wa bili.

"tumeanza bei mpya rasmi ya Maji juzi (01/12/2015) kwa sh 1663 kwa unit moja ya Maji ambayo ni sawa na lita za ujazo 1000. Tulishawaandaa wateja wetu kuipokea bei hiyo kwa kuwaelimisha na pia kupitia njia za mawasiliano za shirika kama vile Tovuti, Magazeti na hata ujumbe mfupi wa simu ya Mkononi ili wajue kiasi cha Maji watakachochajiwa kwa mwezi huu wa disemba" alisema Lyaro.

Mnamo Mwezi novemba 2015. Mamlaka ya udhibiti wa huduma ya Maji na Nishati (EWURA) ilipitisha bei pendekezi ya Maji kwa watumia Maji wa Jiji la Dar es salaam kama ilivyoombwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitka Dar es Salaam (DAWASA) kutoka sh 1098 hadi Tsh 1663 kiwa ni ongezeko la ziaid ya asilimia 50 ya bei ya awali.