Sunday, November 29, 2015

IKULU: Katibu MKUU Wa Wizara ambaye ni Goigoi Ajiondoe Mapema..sasa KUfanya kazi nje ya ofisi na kusikiliza kero za wananchi...HAPA KAZI TU.


IKULU: Katibu MKUU Wa Wizara ambaye ni Goigoi Ajiondoe Mapema..sasa KUfanya kazi nje ya ofisi na kusikiliza kero za wananchi...HAPA KAZI TU.

Joto la utawala wa Rais John Magufuli limebadili utendaji kazi wa makatibu wakuu wa wizara mbalimbali waliozoea kukaa ofisini na sasa wanafanya kazi nje ya ofisi na kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yao.

Wakati hilo likifanyika, Ikulu jijini Dar es Salaam imesema katibu mkuu au mtumishi yeyote wa umma atakayeshindwa kwenda na kasi na mabadiliko ya utendaji kazi katika serikali ya awamu ya tano ajiondoe.

Tamko hilo linalotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alipohojiwa jana  kuhusu kutokuwapo kwa makatibu wakuu wa wizara kadhaa kwenye ofisini zao wiki iliyopita. 
  
Makatibu wakuu wa Wizara kadhaa wamelazimika kuzifunga ofisi zao na kuelekea mikoani kusikiliza kero za wananchi.

Hali ya viongozi hao kuhama jiji na kwenda mikoani imeleta mabadiliko ya utendaji kazi wao baada ya miaka ya nyuma kuzoeleka kutumia muda mwingi ofisini na kuacha kazi za nje kufanywa na waziri, naibu au watendaji wengine.

Baadhi ya wizara ambazo zilitembelewa na kukuta ofisi za katibu mkuu zikiwa zimefungwa ni Uchukuzi, Tamisemi, Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano na Ujenzi.

Baadhi ya wafanyakazi wa wizara hizo ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walisema mabosi wao kwa sasa inakuwa nadra kuonekana ofisini wakifanya kazi kwa kuogopa kuonekana wazembe.

"Hatujawahi kuona katibu anakwenda mikoani kama ilivyo sasa, kila siku anakwenda huku na kule kuangalia miradi na kero za wananchi,"alisema mmoja wa wafanyakazi wa moja ya wizara  hizo.

Hatuna Muda na Katibu Mkuu Goigoi-Sefue
Akitoa kauli ya serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kuanzia sasa katibu Mkuu na mtendaji wa serikali ambaye anafanya kazi kwa kusuasua ajiondoe mwenyewe.

Alisema tayari amefanya kikao na makatibu wote kuwaeleza suala hilo na atakayerudi nyuma hatakuwa na nafasi katika serikali ya awamu ya tano.

"Jambo hilo tumekubaliana kwenye kikao, serikali ya awamu ya tano haitakuwa na utani kwa wale watakaoonekana hawaendi na kasi ya Rais, sasa wanatakiwa kuchagua kama wanataka kuendelea na nafasi  zao au la," alisema Sefue