Sunday, October 04, 2015

TATIZO LA KIUFUNDI HALINA LENGO LA KUWAKOMOA WANANCHI-MRAMBA



TATIZO LA KIUFUNDI HALINA LENGO LA KUWAKOMOA WANANCHI-MRAMBA
Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Dar es Salaam.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kukatikatika kwa umeme linapata hasara ya Sh. Milioni 500 kwa siku na kwamba watanzania waelewe ni matatizo ya kiufundi halina lengo la kuwakomoa wananchi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mtendaji wa  Tanesco, Felichesmi Mramba alisema hali ya kukatika umeme inayoendelea nchini ni kutokana na marekebisho ya baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme na mifumo ya gesi inayomilikiwa na kampuni binafsi inakwamisha upatikanaji huduma hiyo kwa uhakika.
 
Alisema suala hilo halihusiani na siasa bali ni matatizo ya kitaalamu ambayo hata shirika linapata hasara na wakati mgumu kwa kushindwa kuwapatia huduma sahihi wateja wao.
 
"Baada ya bomba la gesi kukamilika, visima viwili kati ya vine vilianza kuingiza gesi kwenye bomba Agosti 22, mwaka huu kule Mtwara na ilifika jijini Dar es Salaam, Septemba 5, mwaka huu … hata hivyo gesi hiyo ilifika ikiwa na msukumo wa bars 2 na kwamba ilichukua wiki mbili kufikia bars 37 kuwezesha kuwasha mitambo ya megewati 90" alisema na kuongeza kuwa.
 
"Mtambo wa Kinyerezi kazi inaendelea hadi wataalamu watakaporidhika kwamba mabomba yote ni masafi na yanaweza kuanza kuwashwa tayari kwa kutoa huduma… kukamilika kwa mitambo hiyo kutatuhakikishia jumal ya megawatio 305 zaidi ya umeme unaopatikana sasa"alisema Mkurugenzi Mramba.
 
Akifafanua zaidi alisema mbali na umeme wa gesi hali ya mabwawa yanayozalisha umeme kwa sasa hayana maji ya kutosha baadhi yanaelekea kukauka.
 
Alitaja mabwawa hayo na kiwango chake cha maji kuwa, Mtera Uwezo wake wa juu ni megawati 800, uzalishaji wake wa sasa ni sifuri (0), Kidatu 204 kwa sasa 27, Kihansi, 180 kwa sasa 51.5 New Pangani Falls, 68 kwa sasa 17, Hale 21 kwa sasa 4 na Nyumba ya Mungu ni 8 kwa sasa 5.5.
 
Alisema shirika linasikitishwa na taarifa za uzushi zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mitambo ya Kinyerezi ni chakavu haiwezi kufanyakazi kwamba siyo kweli zina nia ya kulichafua shirika hilo.