Friday, October 02, 2015

STOP PRESS: RUFAA ZA MRAMBA NA YONA ZAGONGA MWAMBA, KUTUMIKIA MIAKA 2 BADALA YA MITATU, FAINI YA MILIONI 5 YAFUTWA


STOP PRESS: RUFAA ZA MRAMBA NA YONA ZAGONGA MWAMBA, KUTUMIKIA MIAKA 2 BADALA YA MITATU, FAINI YA MILIONI 5 YAFUTWA

Na Mwene Saidi wa Globu ya Jamii

Rufaa iliyokatwa na mawaziri wa zamani  Basil Mramba (kushoto) na Daniel Yonah imegonga mwamba katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam leo, baada ya kuwapunguzia mwaka mmoja na kuwaondolea faini ya milioni 5 na kutakiwa kuendelea kutumikia kifungo cha miaka miwili  baada ya mahakama hiyo kuona hakuna ushahidi wa kuthibitisha shitaka la kusababisha hasara ya Sh. bilioni 11.7.


Kadhalika, mahakama hiyo imesema Mahakama ya Kisutu, ilikuwa sahihi kumwachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja kwa kuwa hakuna ushahidi uliothibitisha kuhusika na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha hasara hiyo.



Hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa mbili saa 3:28 hadi 5:00 na Jaji Projest Rugazia aliyesikiliza rufaa mbili zilizokatwa na pande zote mbili dhidi ya kesi hiyo.



Awali upande wa Jamhuri ulikata rufaa kupinga hukumu ya kumwachia huru Mgonja na utetezi ulikata rufaa kupinga hukumu ya kuwatia hatiani Mramba na Mgonja.
Jaji Rugazia alisema hakuna ushahidi ulitolewa mahakamani kueleza namna gani washtakiwa walihusika kusababisha hasara na kwamba adhabu ya kosa hilo ilitolewa kimakosa dhidi ya washtakiwa.
Alisema kulingana na ushahidi uliotolewa hakuna lawama kwa Mahakama ya Kisutu, kumwachia huru Mgonja dhidi ya mashitaka yaliyokuwa yanamkabili kwenye kesi hiyo.
Pia, alisema haoni kama kuna sababu ya kumhusisha rais (wakati huo Benjamini Mkapa) kwa kuwa alitoa maelekezo kulingana na maelezo aliyopewa na mshtakiwa wa Yona.



"Sioni sababu ya kumtumia rais kwa makosa yaliyotokea kwa kuwa alitoa maekezo kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na mshtakiwa wa pili, Yona... pia hakuna ushahidi uliowaweza kuelezea mahakama namna gani washtakiwa walifanya kosa la 11 la kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7, mahakama hii inatengua adhabu ya kosa hilo na washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka miwili kila mmoja" alisema Jaji Rugazia.
Mapema Julai 6, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, iliwatia hatiani washtakiwa hao na kumwachia huru Mgonja.
Wafungwa hao kwa pamoja  wamekutwa na hatia ya makosa 10 ya kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart ( ASSAYERS) Government Business Corporation kwa ajili  ya kufanya ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini.