TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka wananchi wote waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwenda kupiga kura ya urais, ubunge na udiwani katika vituo walivyojiandikisha kulingana na tamko la sheria ya uchaguzi na si vinginevyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima, mjini hapa, kabla ya kumkaribisha Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe, kufungua mafunzo kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa.
Mafunzo hayo yanawashirikisha pia wasimamizi wa uchaguzi, maofisa uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kutoka mikoa ya Pwani na Morogoro. Alisema hivi sasa kunatolewa tafsiri zinawapotosha wananchi kuwa alimradi ukiwa na kitambulisho cha mpiga kura, hata ukiwa nje ya kituo chako ulichojiandikisha utakuwa na uwezo wa kupigia kura kwa kila mgombea.
Alisema wanaosema hivyo wanapotosha wananchi kwa kuwa sheria ya uchaguzi inatamka bayana kwamba mtu aliyejiandikisha anaruhusiwa kupiga kura katika kituo chake pekee na si mahala pengine.
Alisema walioruhusiwa kupiga kura nje ya kituo walichojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ni wale watakaojaza fomu ya tamko namba 18, ambacho ni kibali cha kumwezesha Mtendaji wa uchaguzi, wakala wa chama cha siasa, askari, wasimamizi wasaidizi na makarani kupiga kura kituo ambacho hawakujiandikisha.
Alisema fomu namba 17 ni tamko ambalo hutumika kwa mpiga kura kuthibitisha utambulisho wake, pale kunapojitokeza mashaka na kwamba hutolewa kwa mpiga kura aliyetiliwa mashaka kuwa amekwisha piga kura yake au hana haki ya kupiga kura.
Alifafanua kwamba Msimamizi atampa tahadhari mtu huyo ya kwamba ni kosa kwa mtu kupiga kura kama hana haki kwa mujibu wa sheria na kwamba anaweza kushitakiwa mahakamani.
"Tamko hili la kisheria inatumika kwa mtu aliyejiandikisha ndani ya kituo husika, picha yake ipo na maelezo yake, lakini kimwonekano wa sura inakuwa tofauti na ilivyo kwenye kitambulisho cha kupiga kura," alisema Kailima.
HABARI LEO