Sunday, September 06, 2015

WAKAZI WA BUGURUNI HATARINI KWA KIPINDUPINDU



WAKAZI WA BUGURUNI HATARINI KWA KIPINDUPINDU

Wakati Dar es Salaam na mikoa jirani ikitikiswa na kipindupindu wakazi wa Ilala jijini hapa wapo kwenye hatari ya kuugua maradhi ya milipuko yanayotokana na kutumia maji yaliyochanganyikana na taka za vyooni yanayotoka kwenye mabomba.



Familia zilizoathirika ni za mitaa ya Ilala, Shariff Shamba na Buguruni ambazo kila zinapofungua maji  kwenye mabomba ya kampuni ya kusambaza maji safi na kuondoa maji taka (Dawasco) zinakutana na maji machafu.

Wakizungumza na gazeti hili walisema maji hayo yana rangi ya damu ya mzee, yanatoa harufu na yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu. Wakati sakata hilo likikosa ufumbuzi, ripoti za kipindupindu jijini Dar es Salaam zinasema hadi sasa watu zaidi ya 400 wameugua na zaidi ya 10 wamefariki dunia.

Mkazi wa eno hilo, Flora Lema, alisema baada ya kuona mabadiliko ya maji hayo walitoa taarifa Dawasco wilayani Ilala na kuahidiwa kuwa kampuni hiyo ingechunguza chanzo.

Licha ya juhudi hizi lakini sikuona mafundi nilikwenda makao makuu ya Dawasco baada ya kusikilizwa waliwasiliana na ofisi za Ilala na mafundi wao wakafika Jumatatu wiki hii, alisema Lema.

Mafundi hao walifika nyumbani kwake na kuchukua sampuli za maji hayo na kurudi kufunga maji ili yasiendelee kutoka. Lakini kilichomshangaza ni Dawasco kufunga maji nyumbani kwake huku wananchi wengine wakikumbwa na tatizo hilo.

Afisa Afya wa Kata ya Ilala, Mary Mkwazi, akizungumza na gazeti hili alisema mara baada ya ofisi yao kupokea taarifa hizo waliwatembelea waathirika na kuwakataza kutumia maji hayo wakati huo huo wakiwahimiza Dawasco kuharakisha uchunguzi ili kubaini chanzo na aina ya uchafu .

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Magembe, alipopelekewa sampuli ya maji hayo na mwandishi wa habari hizi aliahidi kuyawasilisha Dawasco kwa uchunguzi, na kuongeza kuwa si mara ya kwanza kusikia tatizo hilo Buguruni .

Mmoja wa mafundi wa Dawasco Ilala, Ramadhan Mangandale, alisema uchunguzi unaendelea lakini hadi sasa hawajabaini chanzo cha kuchafuliwa maji hayo ingawa kuna hofu kuwa huenda mabomba yamepasuka na maji kuchanganyikana na maji taka.