TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa zaidi kuhusu Mahujaji kutoka Tanzania waliofariki na kujeruhiwa huko Saudi Arabia.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Ubalozi wake mjini Riyadh, Saudi Arabia imepokea taarifa kuwa hadi kufikia tarehe 27 Septemba, 2015 watu waliopoteza maisha kufuatia tukio la mkanyagano (stampede) wa Mahujaji waliokuwa wakielekea Jamarat kutupa vijiwe huko Mina nje kidogo ya mji wa Makkah, lililotokea siku ya Alhamisi tarehe 24 Septemba, 2015 wameongezeka na kufikia 769 na majeruhi 934.
Aidha, Wizara kupitia Ubalozi huo inaendelea kufuatilia hatma ya Mahujaji wa Tanzania waliopotea katika tukio hilo la ajali ambapo hadi sasa Mahujaji wa Tanzania wapatao 50 bado hawajaonekana. Vikundi wanavyotoka Mahujaji hao na idadi yao ni kama ifuatavyo:-
1. Ahlu Daawa-Mahujaji 30;
2. Khidma Islamiya-Mahujaji 16; na
3. TCDO-Mahujaji 4
Vile vile juhudi za Ubalozi kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na viongozi wa vikundi vilivyopoteza Mahujaji wao zimefanikiwa kuutambua mwili wa hujaji mmoja aliyefariki dunia anayejulikana kwa jina la Shafi Khamis Ali kutoka kikundi cha Ahlu Daawa. Kutambuliwa kwa mwili wa hujaji huyo kunafanya idadi ya Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia katika ajali hiyo kufikia watano (5).
Pia, Wizara kupitia Ubalozi wake imepokea taarifa ya kupatikana kwa hujaji mwingine anayeitwa Nasra Abdullah akiwa hai naye kutoka kikundi hicho cha Ahlu Daawa.
Kuhusu majeruhi, taarifa kutoka Ubalozini zinaeleza kuwa, hujaji mmoja aliyejulikana kwa jina la Mahjabin Taslim Khan alipata majeraha yaliyopelekea kukatwa mguu na kwa sasa anaendelea kupata matibabu huku hali yake ikiendelea vizuri.
Ubalozi unaendelea na juhudi za kuwatafuta Mahujaji wengine wa Tanzania ambao bado hawajaonekana kwa ajili ya kubaini wale waliofariki au majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu.
Mahujaji wengine wa Tanzania wapo salama ambapo tarehe 26 Septemba, 2015 walimaliza ibada ya hija na tarehe 28 Septemba, 2015 wameanza safari ya kurejea nyumbani.
Wizara inaendelea kuwaomba Wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
28 Septemba, 2015