Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema pamoja na vitisho ambavyo amevipata kutoka kwa mahasimu wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatarudi nyuma mpaka atakapohakikisha chama hicho kimeng'oka madarakani.
Kadhalika, amesema mwisho wa CCM kukaa madarakani ni mwaka huu kwa kuwa wananchi wameamua kufanya mabadiliko wenyewe.
Aliyasema hayo jana wakati akizindua kampeni za ubunge Jimbo la Ubungo za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema ukiwa ndani ya CCM, ni vigumu kufanya mabadiliko kutokana na mfumo uliopo, lakini hata mtu akiamua kwenda chama kingine kutokana na ukiritimba wa CCM, anakuchukiwa.
Alisema kwa ambavyo ametembea katika mikoa mbalimbali kwa kampeni za kitaifa za mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) anayeungwa mkono vyama shirika vya Ukawa, Edward Lowassa, CCM mwaka huu ni lazima iondoke madarakani.
Alitaja mambo manne ambayo yatachangia CCM kuondoka madarakani kuwa ni pamoja na ukosefu wa Katiba ya Wananchi ya kudhibiti utawala mbovu ambayo alisema Ukawa wakichukua dola, litakuwa jambo la kwanza kuanza nalo na itawapa wananchi mamlaka ya kuwa watawala wa viongozi.
Nyingine ambayo alisema imewafikisha Watanzania katika hali hiyo ya umaskini kuwa ni kukosekana kwa umoja, uzalendo, uadilifu wa utawala ambao umesababisha kutowajibika kwa viongozi na hata kuacha mianya ya rushwa.
Sumaye alisema yeye hajaenda upinzani kwa ajili ya uroho wa madaraka kama wengine wanavyodai, kwa kuwa hagombei nafasi yoyote.
Kwa upande wake, mgombea wa ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Ukawa, Saed Kubenea, alisema endapo wananchi wa Ubungo watamchagua, hawatajuta kamwe kwa kuwa amejipanga vya kutosha kuwasaidia.
Kubenea alisema akiingia madarakani, atashughulikia tatizo la usafiri katika jimbo hilo, tatizo la maji, afya na matatizo mengine.
CHANZO: NIPASHE