Monday, September 14, 2015

SMZ INAZUNGUMZA NA SHELL KUCHIMBA MAFUTA-DK SHEIN



SMZ INAZUNGUMZA NA SHELL KUCHIMBA MAFUTA-DK SHEIN Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya          Kikwete
Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Zanzibar imeanza mazungumzo na Kampuni ya Shell ya Uingereza kwa ajili ya kuchimba mafuta.


Dk Shein alisema hayo jana katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi za CCM Zanzibar zilizofanyika Viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti, Mjini Unguja na kuhudhuriwa na umati wa wananchi wakiwamo marais wastaafu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. "Tayari tumeshaandaa sera na tumetunga rasimu ya mwanzo ya sheria, tunasubiri taratibu nyingine za Serikali yetu hapo baadaye," alisema.



Hata hivyo, alisema utaratibu wa kuchimba mafuta unachukua kati ya miaka mitano hadi saba kabla ya kuanza kunufaika na rasilimali hiyo.
Rais huyo wa Zanzibar alisema lengo la ukombozi wa Tanzania ni kuwawezesha wananchi kuishi vyema na kujiletea maendeleo kama ilivyokuwa dhamira ya waasisi, marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
Alisema kipindi cha miaka mitano aliyokaa madarakani katika awamu yake ya kwanza kilikuwa kigumu kwa kuwa kilihitaji kuvumiliana.
Alisema hakufanya hivyo kwa woga bali, kwa kutumia hekima na kwamba hata akichaguliwa tena atafanya hivyo.

Vigogo wa CCM wanena
Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ambaye hajaonekana kwenye majukwaa ya siasa tangu alipoondoka madarakani miaka mitano iliyopita, alikumbusha namna mfumo wa vyama vingi ulivyoingia nchini mwaka 1992 na kwamba umati mkubwa wa watu kwenye mkutano huo ni sehemu ya maendeleo ya siasa za Tanzania.
Alisema baada ya kutokea machafuko ya kisiasa mwaka 2001 na kusababisha mauaji, timu maalumu iliyoundwa ili kwenda Ulaya kutoa taarifa kwamba tukio hilo lilikuwa ni bahati mbaya.
Alisema miongoni mwa waliokwenda ni Dk Shein na mgombea mwenza wa urais, Samia Suluhu na kwamba wagombea hao wanastahili kuchaguliwa kwa kuwa wamenuia kuleta amani nchini.
Aliwataka wanasiasa wanaotumia lugha za matusi majukwaani kuacha akisema mbinu hiyo haitafanikiwa: "Tafuta lugha nzuri ya kuzungumza na jirani yako hata kama kamwaga maji machafu mlangoni mwako."
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alielezea kushangazwa kwake na umati akisema: "Duh umati wote huu! Haijawahi kutokea." Kisha akasema: "Huu ni mkutano wa aina yake sijawahi kuona namna hii hapa Kibandamaiti lakini naamini kuna maana yake. Uongozi wa nchi utaendelea kuongozwa na CCM."
Aliwaomba wananchi kukichagua chama hicho kwa maelezo kwamba wasipofanya hivyo nchi itakuwa shakani na maendeleo yatakuwa ya mashaka pia.
Makamu wa Pili Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi alisema licha ya wapinzani kuipaka matope CCM na uongozi wa Dk Shein, kiongozi huyo amefanya mambo mengi ya maendeleo jambo linaloashiria ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi mbali ya kusifia umati uliohudhuria uzinduzi huo, aliwaambia wanachama wa chama hicho kuwa muda wa ushindi umefika kwa kuwa kila mmoja anajua namna ya kuuchangia.
Rais mstaafu Benjamin Mkapa alisema ana imani na Dk Shein kwa kuwa amefanya naye kazi pia amefanya kazi na Rais Jakaya Kikwete na wakati wote huo amekuwa mwaminifu.
Rais Jakaya Kikwete alisema tangu ameanza kuhudhuria mikutano katika uwanja huo hakuwahi kuona watu wengi kama hivyo, jambo linaloashiria ushindi kwa chama hicho.
Alisema CCM imeshinda kwa sababu nchi imetulia, ina amani na katika nyakati ambazo Zanzibar ilikosa amani ilitokana na watu fulani ambao wakipewa nafasi amani haitapatikana.
Alisema kama kuna kipindi ambacho Dk Shein amepata misukosuko ni kutokana na vituko vya wapinzani huku akisema Dk Shein ni mzalendo wa kweli mwenye uchungu na Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliponda kauli ya mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba akichaguliwa ataifanya Zanzibar kuwa Singapore akisema mgombea huyo amesahau kuwa chama chake kina zaidi ya nusu ya mawaziri.
"Katika uongozi wake ameshindwa kuileta hiyo Singapore, amegombea mara nne na sasa ni mara ya tano, namwomba waziri amwandalie mafao.
"Ukawa tarehe 25 itageuka kuwa ukiwa, Jamhuri ya Muungano Dk Magufuli na Zanzibar Dk Shein," alisema Kinana.

MWANANCHI.