TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema wananchi wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, hawatapiga kura ya kuchagua mbunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Hatua hiyo, inatokana na kufariki dunia kwa aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mohamed Mtoi (39).
Mtoi, alifariki dunia Jumamosi iliyopita baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kuacha njia na kupinduka kisha kudumbukia kwenye korongo wilayani Lushoto.
Akizungumza na mtandao huu jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema sheria inaruhusu kama mgombea atafariki dunia wakati huu wa uchaguzi uahirishwe.
"Wananchi wa Lushoto hawatapiga kura ya mbunge Oktoba 25, tumeahirisha hadi hapo baadaye tutakapowatangazia na chama husika kitapokuwa kimepata mgombea," alisema Jaji Lubuva.
Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Zubery Mwombeji, Mtoi alipata ajali katika eneo la Magamba Coast, Kata ya Magamba wilayani Lushoto.
Alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Miraj Nuru (43), likitokea Tarafa ya Mlola kwenda Mkuzi baada ya kumaliza shughuli za kampeni.