Hatimaye Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) ya Marekani imeridhia kuipatia Tanzania msaada wa Dola 472.8 milioni (Sh992.8 bilioni), zilizokuwa zimezuiliwa kutokana na jitihada zisizoridhisha za kupambana na rushwa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi waandamizi wa MCC jijini New York, Marekani, mwishoni mwa wiki iliyopita na kuelezwa kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kupata fedha hizo, kikiwamo kigezo cha rushwa kilichokuwa kikwazo.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu, ilisema mabilioni hayo kwa ajili ya awamu ya pili ya MCC, yataanza kutolewa mapema mwakani baada ya wajumbe wa bodi kuidhinisha kwa kura yatolewe Desemba, mwaka huu.
Hatua hiyo ya Bodi ya MCC inaipa ahueni Serikali inayomaliza muda wake kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa umeme wa bei nafuu na wa uhakika, uimarishaji wa taasisi zinazohusika na usambazaji na usimamizi wa nishati hiyo na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi.
Septemba 17, ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa bodi hiyo ilionyesha wasiwasi juu ya mwenendo wa mapambano dhidi ya rushwa yanayofanywa na Serikali, hivyo kuzuia kutolewa kwa fedha hizo hadi itakapofuzu kigezo cha udhibiti wa rushwa katika tathmini ya mwaka 2016.
Hata hivyo, taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete alikutana na ujumbe wa MCC ulioongozwa na Ofisa Mtendaji wake Mkuu, Dana Hyde na kuelezwa kuwa bodi hiyo iliridhika kuwa Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa.
Hyde alimweleza Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, chini ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, iliafikiana kutoa msaada huo.
Ubalozi wa Marekani nchini, nao jana ulitoa taarifa ya mabadiliko hayo ya uamuzi wa Bodi ya MCC.
Balozi Mark Childress alisema amefurahishwa na taarifa kuwa mchakato wa kukamilisha mkataba mpya wa MCC utaendelea.
Wakati huo huo, Tanzania imeunga mkono Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs) na kueleza kuwa malengo hayo ni silaha ya kufuta umaskini duniani katika sura zake zote ifikapo mwaka 2030.
Msimamo huo wa Tanzania ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Rais Kikwete alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalojadili kupitisha malengo hayo mapya chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke Rusmussen.