Monday, September 28, 2015

MAHUJAJI TOKA TANZANIA WALIOKUFA MAKKA WAFIKIA 6 WENGINE 50 HAWAJULIKANI WALIPO



MAHUJAJI TOKA TANZANIA WALIOKUFA MAKKA WAFIKIA 6 WENGINE 50 HAWAJULIKANI WALIPO

Bismillahi rrahmaani rrahiim
Kila sifa njema zinamstahiki Mwenye ezi Mungu Muumba wa viumbe vyote.
Na rehma na amani zimshukie Bwana wetu Muhammad S.A.W, yeye na aali zake wote na maswahaba wake watukufu.
Ammaa baad.
Mwenye ezi Mungu anasema: Sema Muhammad, hayatufiki illa aliyotuandikia Mwenye ezi Mungu, yeye ndie mtawala wa mambo yetu na waumini wamtegemee yeye Mwenye ezi Mungu. Qur,ani Surat Tawba aya 51.
Tamko hili linahusu muendelezo wa taarifa juu ya tukio la kuhuzunisha lilitokea wiki iliyopita Mina Saudi Arabia wakati mahujaji wakielekea kwenye Jamaraat ambapo palitokea msongamano mkubwa (stampede) na kupelekea mahujaji zaidi ya 700 kufariki na mamia kadhaa kujeruhiwa.
Bakwata kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Saudi Arabia tumepata taarifa kwamba maiti mmoja amepatikana ametambulika kwa jina la Shafi Khamisi Ali. Pia Bi Nasra Nassor Abdallah amepatikana akiwa amepata majeraha. Mwenyezi Mungu atawapa tahfif In Shaa Allah.
Kadhalika tumepokea taarifa ya kutopatikana kwa Watanzania 50 ambao walikuwapo Makkah wakati wa tukio hilo. Kati yao 30 walisafiri kupitia taasisi ya Ahlu Daawa, taasisi ya Khidma watu 17 na TCDO watu watatu.
Tunashukuru ubalozi wetu hususan Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Ahmada Sufiani Ali, na wasaidizi wake ambao tumeshirikiana nao katika kupata taarifa hizi.
Tunaendelea kushirikiana na ubalozi wetu pamoja na vyombo vya serikali ya Saudi Arabia.
Bado maafisa wetu wa Bakwata nilionao hapa Makkah wanaendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wetu kwa umakini mkubwa.
Natambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji wetu.
Nachukua fursa hii kwa kuwataka waislamu wote kuwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki na Mwenye ezi Mungu apokee ibada zao na awasamehe madhambi yao na awakusanye katika kundi la waja wema peponi.
Kutokana na mtihani huu kwetu sote, nawaombea dua wafiwa mola awape subra na ustahmilivu na kuwaombea wagonjwa wapate tahfif. Pia nawaomba waislamu wote Tanzania kuwaombea dua wahanga wa mtihani huu.
Mwisho nichukue fursa hii kuwaomba wale wote wenye nafasi ya kuwafariji na kuwasaidia wanafamilia ambao katika ajali hii wamendokewa na nguzo katika familia hizo wafanye hivyo.
Tuwasaidie wanafamilia hawa kwa hali na mali katika wakati huu mzito sana kwao ili tuwapunguzie majonzi na unyonge walionao.
Kwani hapana nguvu wala uweza illa kwa msaada wa Mwenye ezi Mungu na sisi hatusemi illa lile linalomridhisha Mwenye ezi Mungu.

Wabillahi Tawfiiq.
Sheikh Abu Bakari Zuberi
Mufti wa Tanzania
Makkah, Saudi Arabia
28/09/2015