Monday, September 21, 2015

DK, MENGI-TAIFA LINAKABILIWA NA VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI



DK, MENGI-TAIFA LINAKABILIWA NA VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema taifa linakabiliwa na viashiria vya uvunjifu wa amani kutokana na kuwapo kwa mgawanyiko wa kijamii unaosababishwa na watu kupandikiza mbegu za chuki na kukithiri maneno ya uongo.



 
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi kwenye uzinduzi wa Chama cha Wajasiriamali Wanawake (Vowet), Dk. Mengi alisema tatizo hilo ni sawa na saratani inayopaswa kuogopwa na kuomba kila Mtanzania kwa imani yake kuomba kwa Mungu ili upendo uzidi kuimarika na amani idumu nchini.
 
Katika hafla hiyo, Dk. Mengi pia alizindua Chama cha Wajasiriamali Wanawake (Vowet) na kukabidhiwa tuzo ya kumtambua kama mpigania amani na mjasiriamali mwenye mafanikio. Alisema kuongezeka kwa vitendo vya chuki ndani ya jimii, ni ushahidi kwamba upendo na mshikamano uliodumu kwa miaka mingi unaanza kutoweka nchini.
 
"Nawaomba Watanzania kurudisha upendo, kila mmoja kulingana na imani yake tumuombe Mungu, kama wewe ni Muislamu au Mkristo rudini katika vitabu vitakatifu ili kuhamasisha amani na upendo,"  alisisitiza  Dk. Mengi na kuongeza:
 
"Wananchi wamevunjika moyo baada ya kuona viongozi wenye dhamana wanakuwa sehemu ya matatizo kwa kuhusishwa katika vitendo vya rushwa na ufisadi."
 
Alitaka viongozi kuheshimu na kufuata utawala bora kwa kuzingatia uwazi, kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatatua.
 
"Viongozi wawe wepesi kutatua matatizo ya wananchi, kusubiri mpaka maandamano na migomo ni kitu kisichotakiwa kwa sababu vitendo hivyo ni uvunjifu wa amani na vinaweza kusababisha vurugu kubwa nchini," alisema.
 
 "Amani ikitoweka sote tutaumia lakini wanawake, watu wenye ulemavu, watoto na wagonjwa ndio watakaoathirika zaidi, pia itaathiri shughuli zote za uchumi, biashara na shughuli za kiserikali." 
 
Aidha, Dk. Mengi aliwataka wanawake kujikita katika ujasiriamali, akisema utawapa uwezo wa kujitegemea pamoja na kupunguza unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao, kujenga mazingira ya heshima na usawa kati yao na wanaume.
 
Aliwatia moyo wanawake kwa kuwataka  kutokata tamaa na badala yake siku zote wajiamini kwamba wanaweza na watafika mbali kimaendeleo.
 
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Vowet, Maida Waziri, alisema  mkutano huo uliandaliwa kwa ajili ya kuwatia moyo wanawake wajasiriamali pamoja na kuwakumbusha wajibu    wao     katika   kuitunza amani. Alisema wanawake ndiyo msingi wa maendeleo ya Tanzania na  hata katika kipindi cha kupigania uhuru, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwatumia kama sehemu muhimu ya uelimishaji jamii.
 
"Hatutaki kuwa sehemu ya watu watakaovunja amani kwa sababu tunatambua sisi (wanawake) ndiyo waathirika, tunahitaji  uchaguzi mkuu upite ukituacha tukiwa watulivu, wamoja na amani itamalaki," aliongeza kusema Maida.
CHANZO: NIPASHE