Saturday, April 04, 2015

DEREVA WA LORI ALIYESABABISHA AJALI YA BASI LA MAJINJAH NA KUUA WATU 50 AFUNGIWA LESENI



DEREVA WA LORI ALIYESABABISHA AJALI YA BASI LA MAJINJAH NA KUUA WATU 50 AFUNGIWA LESENI
Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi, wamezifungia leseni za madereva sita akiwamo Maga Magazini dereva wa lori lililogongana na basi la abiria la Kampuni ya Majinjah Express na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine 22 kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Sumatra na Polisi jana, hiyo ni moja ya hatua ambayo Serikali imeamua kuichukua dhidi ya madereva waliosababisha ajali kutokana na uzembe, wakiamini kwamba itasaidia kupunguza ajali za mara kwa mara.
Ilielezwa kuwa Magazini (26), mkazi wa Dar es Salaam, Machi 11, mwaka huu alikuwa akiendesha gari aina ya Scania, liligongana na basi hilo katika eneo la Mafinga Changarawe, mkoani Iringa na kuua watu hao 50.
Madereva wengine waliofungiwa leseni zao ni Juma Haule aliyekuwa akiendesha gari lenye namba T 606 BRT Isuzu Forward. Imeelezwa kuwa Machi 22, mwaka huu, aliendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine 22 kujeruhiwa katika eneo la Itamboleo, wilayani Rujewa, Mbeya.
Tangazo hilo linamtaja  Fredy Mng'ong'o dereva wa gari lenye T179 CRG Scania kuwa Machi 17, mwaka huu akiwa katika eneo la Mbuga ya Mikumi akitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya alipokuwa akijaribu kulipita gari lingine, aligongana na gari lenye T670 CFT Mistubish Fuso na kusababisha vifo vya watu wawili.
Wengine waliofungiwa ni Geness Mongi dereva wa basi la Mtei Express aliyesababisha kifo cha mwenda kwa miguu katika eneo la Kiluvya kwa Komba, Dar es Salaam, alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine.
Dereva mwingine ni Jumanne Mwamtemin wa basi la Najims lililoacha njia na kupinduka eneo la Mbwewe Chalinze na kusababisha kifo cha abiria mmoja na wengine wawili kujeruhiwa.
Abubakar Ramadhan aliyekuwa akiendesha basi la Kiruto, anadaiwa kusababisha ajali Machi 25, mwaka huu katika daraja la Ruvu kwa kuendesha kwa mwendo kasi na kumgonga mwenda kwa miguu na kumsababishia kifo. Akizungumza jana, Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alisema wataendelea kuwafungia na kuwatangaza kwenye vyombo vya habari madereva wote watakaobainika kusababisha ajali kwa uzembe.
"Tunaamini hatua hii itasaidia kuwarejesha kwenye hali ya umakini na utulivu madereva wanaopenda kazi zao, madereva wengine wakiona hatua hii tunaimani kuwa watashtuka na kubadili tabia," alisema Mziray.
Alisema kila mwezi Sumatra itakuwa ikiwatangaza madereva itakaokuwa imewafungia leseni zao.