Na Mwene Nantaha
wa Blogu ya Jamii.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoani Pwani (Corefa), Hassani Othman maarufu kama Hasanoo (44) na wenzake leo waliachiwa huru na kisha kukamatwa na kushtakiwa upya kwa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Kadhalika Hasanoo alifutiwa mashitaka matatu ya uhujumu uchumi pamoja na kusafirisha pembe za ndovu kutoka Dar es Salaam kwenda Hong Kong, zenye thamani ya Sh. bilioni 1.1, chini ya kifungu cha 91 kidogo cha (1) mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba.
Hasanoo na wenzake walipandishwa tena kizimbani na kusomewa mashitaka hayo upya. Washtakiwa wengine ni, Hasanoo, washtakiwa wengine ni, Ali Kimwaga, Danstan Mwanga, Godfrey Mwanga, John Mlay, Khalid Fazaidin na Lusekelo Mwakajila.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali, Liliani Itemba na Paul Kadushi. Jamhuri ulidai kuwa, kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, jijini Dar es Salaam na Hong Kong nchini China, kinyume na kifungu cha 384 ya kanuni ya adhabu sura ya 16, kwa pamoja walikula njama ya kujihusisha na biashara ya nyara za serikali bila ya kuwa na leseni inayowaruhusu kufanya hivyo.
Katika shtaka la pili, Kimaro alidai kuwa kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, Dar es Salaam na Hong Kong washtakiwa hao kwa nia ovu walipanga, wakatekeleza, wakasimamia na kuwezesha kifedha kufanyika kwa biashara ya nyara za serikali kwa kusafirisha vipande 569 vya Pembe za ndovu, vyenye uzito wa kilogramu 1330 na thamani ya Sh 1,185,030,000 kwenda Hong Kong.
Ilidaiwa kuwa, katika shtaka la tatu alidai kuwasiku hiyo ya tukio washtakiwa hao walijihusisha na biashara ya nyara za serikali kinyume na kifungu cha 80 na 34 ya uhifadhi wa Wanyama Pori namba 5.
Ilidaiwa pia, washtakiwa hao kwa nia ovu waliendesha biashara hiyo ya nyara za serikali bila ya kuwa na kibali halali kinachowaruhusu kufanya biashara hiyo. Hata hivyo upande huo wa Jamhuri uliwasilisha hati ya DPP ya kuzuia dhamana dhidi ya washtakiwa na uliwasomea washtakiwa maelezo ya awali. Washtakiwa walikana mashitaka na maelezo hayo, kesi imepengwa kusikilizwa Oktoba 6, mwaka huu.