Monday, August 10, 2015

UMEME WA GESI SASA KUANZA MWEZI UJAO



UMEME WA GESI SASA KUANZA MWEZI UJAO
Waziri wa Nishati na              Madini, George
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesema umeme wa gesi utaanza kutumika mwezi ujao baada ya ujenzi wa bomba la kupitisha gesi hiyo kukamilika kwa asilimia 100.

Akizungumza juzi wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa bomba hilo na mitambo ya umeme wa Kinyerezi, Simbachawene alisema bomba hilo limekamilika na liko kwenye hatua ya majaribio.
Alisema hatua mbalimbali za majaribio zilianza tangu Julai 24, mwaka huu na kazi inayofanyika sasa ni majaribio ya kuunganishwa bomba hilo na njia kuu ya umeme ya msongo wa kilovoti 220 wenye urefu wa kilomita nane kutoka kituo cha kupozea umeme cha Kinyerezi hadi Kimara.
"Nafahamu kwa siku za karibuni hali ya umeme katika baadhi ya mikoa siyo nzuri, nawaomba wananchi wawe wavumilivu, kwani tatizo hilo liko katika hatua za mwisho kumalizika," alisema. Simbachawene.
Alisema gesi hiyo kabla haijaanza kutumika yatafanyika majaribio, ikiwamo mitambo ya kuchakata gesi, usafirishaji wa gesi, uwashwaji wa mitambo ya kufua umeme, uunganishaji wa laini ya umeme utakaozalishwa kutoka mitambo ya Ubungo na majaribio ya kusafirisha umeme kutoka katika mtambo wa Kinyerezi kwenda Gridi ya Taifa.
Simbachawene alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lilianza kazi ya upimaji wa mtambo wa Madimba kuhimili kiwango cha gesi inayoingia na kuichakata katika viwango vinavyotakiwa kwa muda wa wiki mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk James Mataragio alisema walishaanza kutoa gesi ardhini na kuipeleka kwenye Mtambo wa Madimba kabla kuisafirisha kwenda Kinyerezi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema mitambo ipo kwenye majaribio, hivyo watalazimika kukata mitambo ya kituo cha Ubungo, Tegeta na Kinyerezi kwa nyakati tofauti wakati wa kuunganisha umeme wa gesi.