Thursday, August 20, 2015

Pasta 'aliyeua' kortini kuzuia asishikwe


Pasta 'aliyeua' kortini kuzuia asishikwe

Chini ya saa 24 tangu kiongozi wa mashtaka nchini Kenya bwana Keriako Tobiko kushauri polisi wamfungulie Pasta James Maina Ng'ang'a mashtaka matatu ya kusababisha mauaji ya bi Mercy Njeri kwa kuendesha gari lake bila kuwa muangalifu , pasta huyo sasa amekwenda mahakamani kuzuia asifunguliwe mashtaka.


Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma nchini Kenya alikuwa amependekeza afikishwe kizimbani kwa kuendesha gari pasi na umakini, kusababisha mauaji, kukosa kuripoti ajali aliyosababisha na kutoa ripoti za uongo.
Kupitia kwa wakili wake Assa Nyakundi na Cliff Ombeta Pasta Ng'ang'a amemuomba Jaji wa mahakama kuu ya Nairobi Weldon Korir, kuzuia asifunguliwe mashtaka yanayomkabili.
Jaji huyo aliagiza karatasi za kesi hiyo ziwasilishwe haraka katika afisi za Inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya na Mkurugenzi wa Mashtaka iliwakutane wote siku ya Alhamisi.

Pasta Ng'ang'a amemuomba Jaji wa mahakama kuu ya Nairobi Weldon Korir, kuzuia asifunguliwe mashtaka

Mkurugenzi wa Mashtaka alikuwa ameahidi Pasta huyo ajibu mashtaka kwa pamoja na afisa mkuu wa polisi katika eneo lilikotokea ajali hiyo huko Tigoni na afisa aliyekuwa akimlinda kabla ya ajali hiyo .
Aidha Simon Kuria aliyefika kortini akidai kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo aina ya Range Rover lililosababisha ajali hiyo katika barabara kuu ya kutoka Naivasha kwenda Nairobi pia atashtakiwa kwa kutoa habari za uongo mahakamani.
Walioshuhudia ajali hiyo wanadai kuwa Pasta huyo alikuwa akiendesha gairi aina ya Range Rover kwa kasi na kuligonga gari la marehemu bi Njeri ana kwa ana.

Pasta Ng'anga anakabiliwa na makosa matatu kuhusu ajali iliyosababisha kifo cha Mercy Njeri

Hata hivyo hakuripoti tukio hilo kama inavyostahili mbele ya sheria za barabarani nchini Kenya ila aliabiri gari lingine na kuendelea na safari yake licha ya kuwa alikuwa ameua kwa mujibu wa taarifa za wale waliofika hapo punde baada ya tukio hilo.
Licha ya kuwa mtu anayefahamika kama Simon Kuria alijitokeza na kusema kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo wakati wa ajali uchunguzi uliofanywa na inspekta mkuu wa polisi ulibaini kuwa huo haukuwa ukweli.
Kauli hiyo ya kumfungulia mashtaka ilitokana na uchunguzi huo na ushahidi wa watu waliofika katika eneo la tukio.
Wakenya wamelalamika na kuishinikiza polisi kufanya uchunguzi upya baada ya kutibua njama ya kuficha ukweli katika kituo cha polisi la eneo la tukio.
BBC.