Wednesday, August 19, 2015

MCHANGO WA MAWAZO: Lowassa ni mfamaji au mpambanaji asiyechoka? -Padri Privatus Karugendo



MCHANGO WA MAWAZO: Lowassa ni mfamaji au mpambanaji asiyechoka? -Padri Privatus Karugendo
Waziri Mkuu wa zamani, Edward              Lowassa
Nimejitahidi nilivyoweza kutoandika chochote juu ya Edward Lowassa. Nilikuwa na sababu kadhaa ambazo siyo lazima kuziandika kwenye makala haya.

Nimeamua kuandika, kwa vile uzalendo umeyashinda mengine yote! Nikiendelea kukaa kimya uzalendo utanishitaki!
Pia, nimeamua kuandika kwa vile Lowassa, ameshindwa kufuata nyayo za wazee wetu; Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Mzee John  Malecela.
Binafsi niko mbali na mawazo kwamba Ikulu ya Tanzania, ni lazima ikaliwe na "wenyewe". Siko huko, maana imani yangu ni kwamba Tanzania ni yetu sote na kila Mtanzania, anaweza kuingia Ikulu. Hatuna uongozi wa kifalme, hivyo sitarajii Ikulu yetu kuwa na wateule fulani.
Ikulu yetu haina chama na wala hakuna chama kilichoandikiwa kuwa Ikulu milele. Hoja yangu ni kumlinganisha Lowassa na wazee waliomtangulia. Namwangalia huyu ndugu yetu asiyechoka kuitamani Ikulu.
Huyu ni kati ya watu waliozipigania sekondari za kata. Kwa nini asipambane bila kuchoka na kuhakikisha sekondari hizi zinaendelea vizuri? Huyu ni mtetezi wa wafugaji, yeye mwenyewe ni mfugaji; kwa nini asipambane bila kuchoka ili kuhakikisha wafugaji wanapata haki zao na wanafuga kisasa?
 Ni lazima apambane bila kuchoka kuingia Ikulu? Kwa nini safari yake ya kuingia Ikulu ni ya udi na uvumba, kufa na kupona! Ni lazima tujiulize. ameshindwa CCM, amekimbilia Ukawa, kwa nini?
Mzee Mwinyi, aliwajibika. Hakusikika popote akijitetea au kulalamika kwamba waliokuwa chini yake ndiyo walimwangusha, hakulalamika kwamba hakupewa nafasi ya kusikilizwa. Alipima uzito wa tukio na na kuamua kujiuzulu bila ya kusukumwa na mtu yeyote yule. Aliwajibika kwa moyo mkunjufu, aliwajibika kwa unyenyekevu mkubwa.
Nina imani alitawaliwa na busara na hekima kubwa. Aliwajibika na kukaa kimya na kuendelea na shughuli nyingine, hadi pale chama chake kilipompendekeza kuwa Rais wa Taifa letu.
Mwalimu Nyerere, alimshambulia Mzee Malecela, waziwazi hadi kufikia hatua ya kuandika kitabu juu yake. Hadi leo hii hatujasikia Mzee Malecela, akimshutumu Mwalimu au kusahihisha kauli ya Mwalimu juu yake. Alikaa kimya na kuendelea na shughuli nyingine. Nina imani naye aliongozwa na busara na hekima. Pamoja na shutuma za Mwalimu, chama chake kiliendelea kumheshimu kwa kumpatia nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara, hadi alipoamua kuacha mwenyewe.
Wazee hawa wawili ni kati ya watu walioonja kupanda,kushuka na kupanda katika siasa za Tanzania. Ni mfano wa kuigwa kwa kuwajibika, kulipenda taifa na kuamini kwamba kuna watu wengine wenye uwezo wa kuliongoza Taifa letu la Tanzania.
Lowassa, pia ameonja kwa namna yake kupanda na kushuka  katika siasa za Tanzania. Alipokuwa Waziri wa Ardhi, jina lake lilivuma Tanzania nzima. Kila mtu alifahamu Lowassa na kumpenda. Alimwagiwa sifa nyingi za ushujaa na utetetezi wa haki ya wanyonge
Mwalimu Nyerere kwa sababu zake alizozifahamu na hakuna wa kuzipuuza, alilishusha jina Lowassa, pale alipomzuia kuchukua fomu ya kugombea  kiti cha urais  kupitia Chama cha Mapinduzi. Pia, mwanzoni mwa Serikali ya awamu ya tatu ya  Benjamin  Mkapa, ilimtupa kapuni. Baadaye  aliibuka tena na kuingia kwenye Baraza la Mawaziri. Yaliyofuata hapo tunayafahamu wote, jinsi alivyovuma tena na kutengeneza mtandao wa nguvu hadi kupata nafasi ya Uwaziri Mkuu.
Richmond, imeshusha tena jina la Lowassa. Bahati mbaya, au labda kwa kushauriwa vibaya amekataa kuiga mfano wa Mzee Mwinyi na Mzee Malecela. Ameamua kutumia vyombo vya habari na washabiki wake katika jimbo lake la uchaguzi, kulalamika na kuweka busara na hekima pembeni.
Kwa nini namuandika?
Nimeamua kuandika baada ya kuona huyu mwenzetu inawezekana si mfamaji, bali ni mpambanaji asiyechoka. Hapana shaka kwamba pamoja kuonyesha kuchoka kimwili, bado ana nguvu za wafuasi. Bado ana watu wengi. Hatuwezi kumpuuza.
Tumeona baadhi ya vigogo wakihama CCM kumfuata, na wengine (ambao utafiti wangu)  unaonyesha ni wengi, wako kimya lakini wanamuunga mkono chini kwa chini na kimya kimya. Anaweza kuwashangaza wengi tarehe ikifika. Huyu si kapi, na mtu anayefikiri kwamba ni kapi, atakuwa ana matatizo ya kuona ukweli.
Ni kweli kabisa kwamba Lowassa, ana haki ya kujitetea, ana haki ya kusikilizwa. Sina tatizo na hilo. Tatizo langu ni pale anapojitetea na kupotosha ukweli. Ni lazima tuhoji kwa umakini; ni kwamba yeye alitaka kuifuta Richmond mara mbili. Maana yake ni kwamba, alikuwa hakubaliani na utendaji kazi wake.
Anakiri  alianza kunusa mchezo mchafu kwenye Richmond. Swali langu kwake, ni je, pale Mkurugenzi wa Takukuru, alipoisafisha Richmond, mbona hatukusikia sauti yake akihoji? Kama alitaka kuifuta mara mbili, anawajibika kuwaelezea Watanzania ni kwanini aliyaamini maelezo ya Takukuru kwamba Richmond ilikuwa safi wakati hata watoto wa shule ya msingi walifahamu na kutambua kwamba Richmond ilikuwa na matatizo?
Bila kueleza hili, kwa vile ameamua kuzungumza, atakuwa anajizika mwenyewe. Wale wanaoimba wimbo wa " makapi" ni bora wakauliza maswali kama haya.
 Lowassa, alisema CCM ina mfumo wake wa kuvuana nguo kwenye vikao vya chama, na  wala siyo bungeni. Maana yake ni kwamba alikuwa akiwalaumu wabunge wa CCM, waliomshambulia bila ya huruma pale bungeni. Pia, alisema kwamba hilo litajadiliwa kwenye vikao vya chama.
Hapa kuna mambo mawili ambayo ni lazima Watanzania wayaangalie kwa umakini: kwanza ni kwamba kuna mambo ya chama ambayo ni lazima yajadiliwe ndani ya chama na kuwa na sauti mmoja ya Chama. Je, ni kweli kwamba suala la Richmond ni la CCM? Ni jambo la wao kujadili wamefunga milango?
Taifa zima lilikuwa kwenye giza, wakati waheshimiwa fulani wakifanya mikataba ya kitapeli. Taifa linapoteza milioni 152,000 kila siku, bado suala hili liwe la CCM peke yao? Wale wanaoimba wimbo wa " makapi" haya ndiyo ya kuwaelezea Watanzania.
 Inawezekana Lowassa ni mfa maji au  ni mpambanaji asiyechoka? Na je, anapambana kwa lipi? kwa vile hakuna Watanzania wengine wa kukikalia kiti cha Urais?
MWANANCHI.