Wednesday, August 19, 2015

JICHO LA TATU: TERRY, COSTA WANAITESA CHELSEA


JICHO LA TATU: TERRY, COSTA WANAITESA CHELSEA

chelsea

Na Simon Chimbo;

Ligi kuu soka nchini England maarufu kama EPL imeanza na wikendi hii itaingia katika mzunguko wa tatu mara baada ya kila timu kucheza michezo miwili wiki mbili zilizopita na kushuhudia mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Chelsea wakiambulia point 1 katika michezo yake miwili ya awali.

Kwa mtazamo wangu, sio ishu kubwa kwa Chelsea kuanza taratibu kiasi hiki kwani walipata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Swansea, timu ambayo msimu uliopita ilizifunga klabu za Arsenal na Manchester United katika michezo yote ya nyumbani na ugenini. Kwa hivyo kwa Chelsea kutoa sare ni moja ya matokeo ya mchezo na hasa ikizingatiwa kuwa Chelsea walicheza pungufu kwa zaidi ya dakika 30 mara baada ya Thibaut Qourtois kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Chelsea wakafungwa mabao 3 na Manchester City katika uwanja wa Etihad wikend iliyopita katika mchezo ambao walizidiwa mbinu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.

Sitaki kuzungumzia matokeo ya michezo hiyo miwili ya awali kama agenda ya kuwashusha viwango msimu huu, la hasha! Najaribu kuwatizama katika muono mrefu wa hadi mwisho wa msimu.

Msimu wa mwaka jana waliotwaa ubingwa, Chelsea walianza kwa kushinda mfululizo katika mechi za awali na hata kutwaa ubingwa katika staili ya aina yake kwa kupoteza mechi zisizo zidi tatu.

Tujaribu kujiuliza nini kilikuwa siri ya mafanikio ya mwaka jana? Kwanini msimu huu hawaonekani kuwa na kasi ile ya mwaka jana?

Nacho kiamini msimu uliopita ni kwamba kusingekuwa na maswali kama John Terry angetangazwa mchezaji bora wa mashindano(ligi), kutokana na ukweli kwamba pamoja na uwezo wa wachezaji wengine kikosini  hapo kufanya vizuri, lakini Terry alikuwa ni nguzo na uti wa mgongo wa mafanikio ya Chelsea mwaka jana.

Amefikisha umri wa miaka 34 hivi sasa, moyo unataka, mwili hauwezi. Ligi kuu ina kasi ya ajabu, inahitaji walinzi wepesi wakukimbizana na akina Alexis Sanchez na Sergio Aguero.

Kocha wa Chelsea Jose Mourinho alimtoa nje kwa mara ya kwanza tangu arudi mara ya pili kuifundisha klabu hiyo katika mchezo dhidi ya Manchester City wikend iliyopita. Lakini hilo pia linathibitisha mwanzo wa mwisho wa zama za kiranja huyo wa Stamford Bridge.

Mchezaji mwingine muhimu kuliko wengi wanavyoweza kumfikilia, ni mshambuliaji Diego Costa. Kocha Harry Redknapp ana msemo wake na filosofia yake ya kuamini katika kushambulia kama njia mbadala ya kuzuia.

Msimu uliopita, mshambuliaji huyo aliifungia Chelsea magoli 20 na kuisaidia timu yake kuukaribia ubingwa hata alipoumia baadae, Chelsea haikuwa na kazi kubwa sana ya kumalizia mkia kitu kilichochagizwa sana na morali na saikolojia ya timu kushinda.

Umuhimu wa Diego Costa kikosini hapo ni mkubwa sana hasa nikikumbuka Chelsea walivyo unga unga kupata matokeo mwishoni mwa msimu wa mwaka jana mshambuliaji huyo akiwa majeruhi.

Hali ya majeruhi ya mara kwa mara pamoja na kukamiwa kiasi na walinzi msimu huu, kunampa wakati mgumu Diego Costa kuisaidia timu yake kama mwaka jana.

Nini kifanyike? Binafsi nimeshangazwa sana na kitendo cha Mourinho kujiamini hata asisajili wachezaji wa kiwango cha dunia kuimarisha na kuchukua tahadhari ili kutetea ubingwa msimu huu.

Mourinho ameimba mara kadhaa kuhusu kutaka kimsajili mlinzi chipukizi wa Everton, John Stones lakini bado amebaki kimya akitarajia msimu wa maajabu tena kwa John Terry, ni ngumu kutetea ubingwa.

Aidha kuhusu kufidia, majeraha ya Diego Costa, Mourinho alisita kitu gani kutoa pauni 40m kumsajili Griezman kutoka Atletico Madrid ili aongeze changamoto na ubunifu katika eneo la ushambuliaji?

Hayo pamoja na kutokuwa na imani na vijana wa academy, kuja kuwasaidia wakina Cesc Fabregas, Oscar na Ivanovic wanaoonekana kuchoka sana msimu huu, kunanifanya nisiamini nguvu ya Chelsea msimu huu kutetea ubingwa wao sanjari na kufanya vizuri katika michuano mingine.

Wiki iliyopita kuna mchambuzi mmoja nchini England aliandika kwamba kocha Jose Mourinho hivi sasa, amekuwa na stress kutokana na kushindwa kusajili wachezaji wazuri kitu kinachomsababisha hata kugombana na madaktari wa timu kwa sababu zisizo na mashiko.

Alex Ferguson, alikua akiweza kutetea ubingwa hata hadi mara tatu, tutasubiri kuliona hilo kwa Mourinho mwisho wa msimu, kwani katika mpira, lolote linawezekana.

Chelsea, wanaweza kubadilika haraka na kuanza kupata matokeo ambayo yanaweza wapa chochote msimu huu kwani kuna michezo 36 imebakia mbele yao, na ligi kuu nchini England ni ligi ya kipekee zaidi ulimwenguni.

Asalam Aleikum.

chimbo445@gmail.com