Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kitengo cha moyo ameruhusiwa kurudi nyumbani.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Chadema, Tumain Makene, Mbowe aliruhusiwa jana saa 6:00 mchana baada ya madaktari kuridhika kwamba afya ya kiongozi huyo ipo vizuri.
"Ameruhusiwa leo (jana) baada ya madaktari kuridhika kwamba afya yake imeimarika na ameenda nyumbani kwa mapumziko," alisema Makene.
Juzi daktari bingwa wa moyo katika hospitali hiyo, Dk. Shem Sanga, alisema Mbowe alipokelewa hapo na kufanyiwa vipimo ambavyo vilionyesha kwamba alikuwa anasumbuliwa na tatizo la uchovu wa mwili uliosababishwa na kufanya kazi mfululizo bila kupumzika pamoja na kutopata chakula cha kutosha.