Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kuwa linaendelea kuboresha miundombinu kwa kuifanyia matengenezo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na mikoani ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora ya nishati hiyo.
Akizungumza na NIPASHE, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin, alisema kuna baadhi ya maeneo uboreshaji wa miundombinu unaendelea ikiwamo kukata matawi ya miti na kuondoa nguzo zilizooza.
"Hatuna upungufu wowote wa umeme matengenezo ya kuboresha miundombinu yanaendelea ikiwamo kukata matawi ya miti na kubadili nguzo zilizokwishaoza," alisema Severin.
Aidha, alisema kwa sasa hali ya upatikanaji wa umeme inaridhisha kutokana na juhudi za dhati za kuboresha miundombinu zinazoendelea kufanywa na shirika hilo.
Adrian alisema Tanesco tayari imeshakamilisha matengenezo vituo vidogo vya kupoozea na kusambaza umeme vya Gongo la Mboto, Kurasini, Mbagala na katikati ya Jiji.
Aliongeza kuwa shirika hilo litaongeza vituo vidogo katika maeneo ya Mwananyamala, Muhimbili na Bahari Beach.
Alisisitiza mpango wa uboreshaji miundombinu ni endelevu na umelenga kuwafikia wateja nchi nzima.
Aliwataka wateja kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha matengenezo kwani nia ya kufanya hivyo ni kwa ajili ya kutaka mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine ipate umeme wa uhakika zaidi.
CHANZO: NIPASHE