Serikali imesuuza roho za wastaafu nchini kwa kuwaongezea pensheni kutoka Sh. 50,000 wanayopata sasa hadi Sh. 100,000 kwa mwezi.
Hata hivyo, serikali imekataa kuondoa tozo la Sh. 100 kwa kila lita ya mafuta fedha zitakazoelekezwa katika miradi ya umeme vijijini (Rea) na miradi ya maji vijijini.
Katika Bajeti iliyosomwa Juni 11, mwaka huu, serikali ilipendekeza nyongeza ya pensheni kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 85,000 kwa mwezi.
Aidha, tozo ya mafuta ya dizeli na petroli kutoka Sh. 50 hadi 100 kwa lita na mafuta ya taa kutoka Sh. 50 hadi 150 kwa lita ili kuondoa uchakachuaji.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, akijibu hoja mbalimbali za wabunge jana alisema jumla ya wabunge 98 walichangia mjadala moja kwa moja na wengine 13 kwa maandishi.
Alisema kwa kushirikiana na Kamati ya Bajeti, wametafakari michango ya wabunge 17 na kuona kiasi cha pensheni kilichoongezwa na serikali, bado hakitoshi na kwa kuzingatia kuwa ni wazee walioshiriki jitihada za kuleta maendeleo na kulifikisha taifa hapa lilipo.
"Serikali yenu imetafakari kwa makini, imekubali kuongeza ikiwa ni ongezeko la asilimia 100, tunatambua, tunathamini michango ya waliochangia taifa hili, tunatambua bado maisha ni magumu, lakini serikali yenu iko hapa itaendelea kufanya tathmini na mapato yakiridhisha, wataendelea kuongezwa," alisema Waziri Mkuya na kuongeza:
"Kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, wastaafu wa kima cha chini watatoka Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000...tutaimarisha mifumo yetu kuhakikisha wanaopunjwa, wanaokosa fedha zao, wananyanyaswa na watendaji, inakuwa thabiti pale alipo anapata pensheni yake."
Waziri huyo alisema wapo watendaji ambao wanashindwa kutoa majibu sahihi kwa wazee wanaofika Hazina na wanachukuliwa hatua na wataendelea kuchukuliwa kwa kuwa ni haki ya wazee na siyo upendeleo kwa kuwa wamechangia maendeleo ya taifa.
MAFAO YA WAZEE
Alisema hoja ya mafao ya uzeeni ilichangiwa na wabunge 14, serikali imejipanga kuwatambua wazee kote nchini kwani kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wapo milioni 1.2 na kwa sasa kuna ongezeko zaidi hadi mwaka huu kwani kuna waliofikisha umri na wengine wamefariki dunia.
"Kwa idadi hiyo tukisema tulipe kila mmoja Sh. 10,000 kila mwezi, tutahitaji zaidi ya Sh. bilioni 140, lakini hatujui makazi yao yalipo, hivyo kwa mwaka 2015/16, tunatoa fedha kwa maofisa wetu waende kuwatambua mahali walipo, tuwawekee mfumo ambao watapata fedha zao walipo," alifafanua.
Alisema siyo wazee wote waliokuwa serikalini, lakini walichangia Pato la Taifa kwa shughuli zao kwenye sekta mbalimbali na kilio chao kimesikika na yote ni utekelezaji wa sera ya mafao kwa wastaafu.
Mkuya alisema serikali inafanya hivyo kwa kuwa kuna ripoti ya pensheni zinazopelekwa, lakini wahusika hawapati kutokana na mifumo na maofisa ambao siyo waaminifu wamekuwa wakishirikiana na benki kuchukua fedha hizo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuya, kuna kiasi cha Sh. bilioni sita zilichukuliwa kwa wazee bila kujua.
"Tunaomba maofisa wetu watakapokuja popote walipo, muwape ushirikiano, mueleze jinsi gani fedha hizo zitawafikia, fedha hizo tumeshazitenga, baada ya kutoka hapa tunaweka maofisa wetu na ndani ya miezi sita, kazi itakuwa imeisha na tutaanza kulinda ndani ya mwaka huu wa fedha, tuna dhamira nzuri ila tunataka liende kwa ufanisi," alifafanua.
TOZO YA MAFUTA
Waziri huyo alisema wabunge 28 walichangia hoja hiyo sawa na asilimia 27 ya wabunge.
Waziri Mkuya alisema lengo la tozo hilo ni kuwashirikisha wananchi katika kuchangia maendeleo yao.
Aidha, alisema umeme utawafanya wafanyabiashara kupeleka huduma vijijini na kwa tozo hiyo itapatikana Sh. bilioni 276 kwa mwaka.
Alifafanua kuwa kutokana na tatizo la maji, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 90 zitaelekezwa kwenye mfuko wa maji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini.
Alisema kutokana na athari ya uchakachuaji ambayo iliikosesha serikali takribani Sh. milioni 600, serikali imeongeza tozo ya mafuta ya taa ili kuhakikisha dizeli na petroli hazichakachuliwi.
"Fedha hizi haziendi `ku-balance' bajeti ya serikali, bali zinakwenda kupeleka umeme vijijini, kila mbunge aliyesimama hapa alidai umeme kwenye vijiji vyake. Tuna takwimu za utafiti kuwa kutokana na `balance' iliyowekwa miaka ya nyuma, matumizi ya mafuta yamepungua lita milioni 1.8 kwa siku mwaka 2010 hadi lita 130,000. Ni dhahiri hata wananchi wameondokana na matumizi ya mafuta ya taa," alisema.
Waziri Mkuya alisema ni lazima umeme uende vijijini kwa kuwa siyo kwa kuwashia taa bali ni fursa za kiuchumi kwani wakielimishwa vizuri watatengeneza ajira na kuajiri wengine pamoja na kujipatia kipato.
"Vijijini kuna fursa, tukiweka miundombinu vijana ambao wanakimbilia mijini watarudi vijijini kutumia umeme kujitanua kiuchumi, nchi haiwezi kuendelea iwapo tutaangalia upande mmoja wa shilingi, ni lazima changamoto zingeuzwe kuwa fursa, tusifanye uchumi ndiyo ajenda ya kisiasa, " alisisitiza.
Alisema kila mwaka kuna ongezeko la watu la asilimia tatu, hivyo lazima kuandaa fursa za miundombinu, maji na barabara ili waliopo mjini waende vijijini.
"Tunachokitaka kwa mwananchi ni Sh. 100, fedha yote itakayokusanywa itakwenda eneo hilo, wananchi msichukulie hii ni adhabu, mwananchi ni lazima asimamie maendeleo yake kwa mchango wake, uchumi wako utategemea mchango wako," Waziri Mkuya alisema na kuongeza:
"Wafadhili wanatusaidia kwa sababu wanachukua kodi za wananchi wao, kama tuna uchungu wa maendeleo ya nchi, ni lazima mwananchi achangie upatikanaji wa umeme ni asilimia 40 ili mwananchi ahoji maendeleo ya nchi, ni lazima achangie maendeleo."
Aidha, aliviomba vyombo vya habari kuelimisha wananchi juu ya nia njema ya serikali kwa wananchi kuchangia maendeleo yao.
KUPOROMOKA KWA SHILINGI
Akizungumzia kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania, Waziri Mkuya alisema kwa sasa Gavana anaingiza katika soko la fedha kwa wiki Dola milioni 10.
Alisema tangu utaratibu huo uanze, zimeshauzwa Dola milioni 400 katika soko na hivyo upatikanaji wa Dola kuwa na nafuu tofauti na awali.
Waziri Mkuya alirudia kauli yake kuwa Shilingi inaporomoka kutokana na kuimarika kwa uchumi wa Marekani na sarafu nyingi zimeathirika na Shilingi ilibaki tulivu kwa miaka mitatu.
"Tusifanye siasa kwenye jambo hili, ni lazima tukubali kuwa kuporomoka kwa mapato na mauzo nje ya nchi ikilinganishwa na mahitaji ya kununua bidhaa kutoka nje ya nchi ni sababu, tunaagiza vijiti na leso nje ya nchi, tunaagiza zaidi kuliko kuuza, inaathiri mapato yetu," alisema na kuongeza:
"Sababu nyingine ni gawiwo la nje limesababisha Dola itoke nje zaidi, serikali inalipa zaidi malipo ya nje. Tunaweza kupunguza, hivi karibuni Gavana wa Benki Kuu amechukua hatua mwisho wa mwezi tutaona mabadiliko, lakini ukweli ni kuwa kuwapo kwa Shilingi nyingi katika mzunguko wa benki kumeathiri."
Alisema wafanyabiashana na wawekezaji wanapoona nchi za Afrika zinaingia katika uchaguzi, huondoa fedha zao nchini, hivyo kuimarika mwa Shilingi ni jukumu la kila mtu na siyo la serikali pekee.
Alisema kwa sasa ni asilimia 0.1 ya biashara zinafanyika kwa Dola na kiuchumi ni ndogo sana, asilimia 3.2 ya wafanyabiashara wananunua kwa Dola.
Hata hivyo, Waziri Mkuya alisema serikali itafanya uchunguzi mwingine kama kuna matumizi holela ya Dola.
"Hatuwezi kupiga marufuku kabisa matumizi ya Dola, tutarudi miaka ya 80 ambayo ilikuwa ni dhambi kuwa na Dola, baada ya mazingira ya sasa kuna ushamiri wa biashara, ila tunachukua hatua na wanaokiuka, kama tutabana sana wengine watazichukua kwa njia ya panya na kuziondosha nchini, bora mzunguko wa kihalali na tutaweza mazingira sahihi, fedha za kigeni tunazihitaji, utalii ndiyo unaongoza," alisema.
EFD's
Waziri Mkuya alisema matumizi ya mashine za kielektroniki kutoa stakabadhi (EFDs), hakuna mbadala, ni lazima na serikali itaendelea kuchukua hatua kwa wanaokwepa kutumia mashine hizo.
KUPUNGUA KWA UMASKINI
Alisema ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia saba ukilinganisha na kuondoa umaskini kwa wastani wa asilimia mbili, haviendani, sekta ya kilimo inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 70 imechangia kwa asilimia nne, jambo ambalo linaonyesha mchango wa sekta umekuwa mdogo na kinachofanyika ni kuongeza tija kwenye kilimo na upatikanaji wa huduma za jamii.
Waziri Mkuya alisema kwa mujibu wa utafiti, kwa ujumla umaskini umepungua kwa asilimia 6.2 kwa miaka mitano.
Alisema kwa sasa pengo la aliyenacho na asiyenacho limepungua kutoka asilimia 0.37 mwaka 2007 hadi asilimia 0.34 mwaka 2012 na kwa sasa linapungua zaidi ambapo pia wastani wa kuishi kwa Mtanzania pia umeongezeka kutoka miaka 42 hadi miaka 61 mwaka 2012.
UPIGAJI KURA
Wabunge waliopiga kura kupitisha bajeti hiyo ni 294 ambapo 219 walisema `Ndiyo' na 74 walisema `Hapana' huku kura ya Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi, kutotoa uamuzi.
Aidha, wabunge 59 wakiwamo mawaziri watatu, hawakupiga kura, huku Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, akisema `Hapana' na kuwafanya wabunge wa Kambi ya Upinzani kushangiliwa.
Mara kadhaa, Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), amekuwa akitofautiana na wenzake wa Kambi ya Upinzani unapofikia uamuzi katika masuala mbalimbali ndani ya Bunge tofauti na alivyofanya jana.
Aidha, Spika alitangaza bajeti hiyo imepitishwa kwa asilimia 83.
Baada ya upigaji kura, Muswada wa Kuidhinisha Matumizi kutoka Mfuko wa Fedha wa Serikali, ulisomwa kwa mara tatu na leo utaanza kujadiliwa.
MBOWE
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni, Freeman Mbowe, alisema wamechakachua matokeo kwani kwa hesabu ni kuwa bajeti imepitishwa kwa asilimia 74.4 na Watanzania wameona yaliyotokea hivyo wananchi wafanye uamuzi kwenye sanduku la kura ili kuongeza wabunge wengi wa upinzani.
MBATIA
Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha, James Mbatia, alisema serikali inatoa maneno mazuri na matamu ya kuwahadaa Watanzania.
Mbatia alisema kwa msingi huo, Watanzania wanapaswa kupima kwa miezi minne iliyobaki ya serikali na kufanya uamuzi sahihi kwenye sanduku la kura.