Wednesday, June 24, 2015

Mwinyi, Mkapa kuwajadili wakina Membe, Lowassa...Waitwa pia Malecela, Karume, Dk. Salmin, Msekwa athibitisha kuandaa kikao.



Mwinyi, Mkapa kuwajadili wakina Membe, Lowassa...Waitwa pia Malecela, Karume, Dk. Salmin, Msekwa athibitisha kuandaa kikao.
Pius Msekwa.

 Wakati joto la kusaka nafasi ya kuteuliwa kuwania urais kwa tikiti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) likiwa linazidi kupanda, Baraza la Ushauri wa Wazee linajipanga kukutana baada ya kikao kilichokuwa kifanyike leo kuahirishwa.
Katibu wa Baraza hilo, Pius Msekwa, alituambia jana kuwa kikao cha leo kimeahirishwa kutokana na baadhi ya viongozi wakuu wa chama kuwa safarini, kwani walikuwa wamewaalika kwenye mkutano wao uliokuwa ufanyike jijini Dar es Salaam.
 Kikao hicho ni mahususi kwa ajili ya ushauri juu ya watia nia 39 wa urais waliojitokeza kutaka kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Ingawa Msekwa hakusema tarehe mpya ya kukutana ni lini, lakini kuna taarifa kwamba litakutana baada ya tarehe ya mwisho ya kurejesha fomu za kuwania urais Julai 2, mwaka huu.
Baraza hilo linaloundwa na wenyeviti wa CCM na makamu wake wastaafu, linatarajiwa kutoa mapendekezo yao kuhusu namna bora ya kumpata mgombea wao.
Wanaounda baraza hilo kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012 katika katiba yake; ni marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi (mwenyekiti), Benjamin Mkapa (mjumbe), Amani Abeid Karume (mjumbe) na Dk. Salmin Amour (mjumbe).
Wengine ni Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
Mkutano huo wa Baraza la Wazee CCM ni utangulizi wa mfululizo wa vikao vingine vya chama hicho vitakavyoanza Julai 5, mwaka huu.
Msekwa alipoulizwa jana kwa njia ya simu kuhusiana na taarifa hiyo alisema: 
"Tumelazimika kukiahirisha kikao chetu, lakini tutakifanya hapo baadaye kwa sababu kuna baadhi ya viongozi wa juu wa chama wako safarini. Siyo kweli kwamba kesho (leo) tutakutana, ila mkutano utakuwepo baada ya wao kufika Dar es Salaam," alisema. 
Ingawa Msekwa hakuwataja viongozi wa juu wa chama hicho walioko safarini lakini ambao wapo safarini ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete ambaye aliondoka nchini wiki iliyopita kwenda India kwa ziara ya siku nne.
Viongozi wengine wa kitaifa wa CCM ni Makamu wenyeviti Zanzibar na Bara. Hao ni Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Philip Mangula (Bara). Mwingine ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye yupo katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
 Kikao cha NEC cha Februari 12, 2012 ndicho kiliridhia mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa Baraza hilo.
 Kulingana na mabadilko hayo, Baraza la Wazee litakuwa majukumu ya kuwashauri watendaji wakuu wa CCM hasa katika masuala makubwa, mazito na nyeti yanayogusa mustakabali wa taifa.
 Maamuzi ya kuundwa kwa baraza hilo chini ya uongozi wa Rais Kikwete, liliwaondoa viongozi hao wastaafu kuwa wajumbe wa vikao vikuu vya chama vya maamuzi. Vikao vya maamuzi ni Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mkutano Mkuu.
Hata hivyo, wazee hao wanaweza kuhudhuria vikao hivyo endapo tu wataalikwa.
 Awali viongozi hao wastaafu walikuwa wajumbe wa vikao hivyo vya maamuzi.
Mbali na Baraza la Ushauri la Wazee, vikao vingine ambavyo viko katika maandalizi ya kukutana ni Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakayokutana Julai 7 na Kamati Kuu (CC) itakayokutana Julai 8, chini ya Rais Kikwete, ikifuatiwa na kikao cha NEC Julai 9, mwaka huu.
Mchakato wa kumpata mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu utahitimishwa Julai 11 mwaka huu na Mkutano Mkuu wa Taifa CCM ambao ni maalum kwa ajili kulipigia kura jina la mgombea mmoja kati ya watatu.
 Kuundwa kwa baraza hilo kumesababisha viongozi hao wastaafu kutoingia katika vikao vya juu vya maamuzi ya chama kama ilivyokuwa zamani.
MAANDALIZI YAPAMBA MOTO
Wakati hayo yakijiri, hekaheka za maandalizi ya kuanza kwa vikao vya juu vya maamuzi vya CCM yameshika kasi mjini hapa baada ya kushuhudia ukumbi wa mikutano wa NEC ukiwa unaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kuvunjwa; huku majengo mengine ikiwamo White House likiwa linakarabatiwa kwa miundombinu yake kupakwa rangi.