Imeripotiwa kutoka mkoani Simiyu katika Wilaya ya Bariadi kuwa Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo Bw. Ponsian Nyami amemuomba Rais Jakaya Kikwete asimwonee huruma na badala yake atengue uteuzi wake kwa maana ameshindwa kusimamia ujenzi wa maabara katika wilaya yake.
Aliyasema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Elaston Mbwilo katika kikao cha majumuisho baada ya kutembelea maabara hizo na kubaini utekelezaji wake ni asilimia 10 tu.
Kabla ya kauli ya Nyami, Mbwilo alitoa lawama kwa DC kwa kushindwa kusimamia ipasavyo agizo la Rais na kueleza kuwa ndani ya Mkoa, Wilaya hiyo ndiyo ya mwisho katika utekelezaji wa agizo husika.
Hata hivyo Mkuu huyo mkoa alisema kuwa viongozi pamoja na watendaji wameshindwa kutekeleza agizo hilo ikiwa pamoja na miundombinu hasa barabara ndani ya wilaya hiyo kuwa chini ya kiwango, ambapo alimtaka Mkuu wa wilaya kuwachukulia hatua watumishi wote walisababisha hali hiyo.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa naye aliutupia lawama uongozi wa Wilaya hiyo kwa kushindwa uwajibka, huku akieleza kuwa maabara zilizojengwa ziko chini ya kiwango.
Baada ya viongonzi hao kuongea, Mkuu wa Wilaya, Nyami alisema:
"Namuunga mkono Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala Mkoa. Ni kweli tumefanya vibaya, makosa haya ni makosa yangu mimi na wala sina haja ya kuomba msamaha. Niko tayari kuwajibishwa kwa lolote lile na kwa wakati wowote maana nilipoteuliwa nilihaidi kuwa nitaisimamia na kuiheshimu, sasa naona nimeshindwa na usinionee huruma. Nakiri nimeshindwa."
Nyami alibainisha kuwa yeye kama kiongozi Mkuu ndani ya wilaya hiyo haoni haja ya kuonewa huruma, kutokana na kushindwa kusimamia ujenzi huo ikiwa pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi wake.