MIILI zaidi ya watu waliokufa katika mafuriko ya mvua inayoendelea kunyesha Dar es Salaam, imeongezeka na kufikia 12 akiwemo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kigogo mwenye umri wa miaka 13.
Katika tarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa vyombo vya habari ilisema kuwa wamethibitisha vifo vya watu hao.
Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova alimtaja mwanafunzi aliyekufa kutokana na mvua hizo kuwa ni Valerian Eradius, mkazi wa Mburahati kwa Shebe aliyefariki dunia Mei 10, mwaka huu baada ya kuangukiwa na ukuta.
Kova alisema ukuta huo ulianguka kutokana na mvua zilizokuwa zinanyesha jijini na kwamba mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Pia alifafanua kuwa Mei 9, mwaka huu, maeneo ya bonde la mto Mkwajuni katika mtaa wa Makuti, wilayani Kinondoni, mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40-45 alikutwa akiwa amekufa.
Aidha, mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 38 ambaye jina, umri wala makazi yake hayajajulikana mara moja ameopolewa katika tope jana maeneo ya Magomeni Suna katika bonde la Mto Msimbazi akiwa tayari ameshaaga dunia.
Alisema kuwa miili hiyo inaendelea kupatikana kwa jinsi maji yanavyoendelea kupungua kutokana. Kabla ya taarifa hiyo, watu tisa waliripotiwa kufa maji kutokana na mvua hiyo kubwa iliyonyesha mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha pia uharibifu wa mali na miundombinu, huku maelfu wakiachwa bila makazi.