Mkuu wa zamani wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Tabora, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Bhoke Bruno na polisi wawili, wamefikishwa mahakamani kujibu shitaka la upotevu wa bunduki nane aina ya Sub Machine Gun (SMG) mali ya Jeshi la Polisi.
Walifikishwa jana katika Mahakama ya Mkoa wa Tabora.
Washtakiwa wengine waliofikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Issa Magoli, ni Koplo Iddi Abdallah na Mwinyi Gonga, wa Kikosi cha FFU Tabora.
Akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali, Juma Masanja, alidai kuwa washtakiwa wote watatu wanakabiliwa na shitaka moja la kutochukua tahadhari stahiki katika utunzaji wa silaha.
Alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Aprili, mwaka jana na Aprili, mwaka huu wakiwa waajiriwa wa Jeshi la Polisi Kikosi cha FFU Tabora.
Wakili Masanja alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja walishindwa kutumia njia za kiusalama katika utunzaji wa silaha na matokeo yake bunduki nane aina ya SMG ziliangukia katika mikono ya watu ambao si wamiliki halali wa silaha hizo.
Watuhumiwa wote walikana shitaka na kurejeshwa mahabusu baada ya kunyimwa dhamana kutokana na Wakili wa Serikali kupinga dhamana kwa hofu ya kuingilia upelelezi pale watakapokuwapo nje.
Hakimu Magoli aliamuru washtakiwa hao warejeshwe tena mahakamani hapo Mei 21, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. CHANZO: NIPASHE