Saturday, May 30, 2015

Mtihani wa Lowassa uko CCM, kwa wananchi mteremko.



Mtihani wa Lowassa uko CCM, kwa wananchi mteremko.

Leo Mbunge wa Monduli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa (pichani), atatangaza rasmi kusudio la kutaka kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho. Hafla hiyo itafanyika jijini Arusha.
 
Gazeti hili lilifika jimboni Monduli na kuzungumza na baadhi ya wapiga kura wake na kadha nyingine zilizomo jimboni humo, kumhusu Mbunge huyo na azma yake ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi wa nchi.
 
Ikabainika kuwa, licha ya kuwapo hisia tofauti zinazomhusu Mbunge wa Monduli mkoani Arusha, Edward Lowassa katika mkakati wa kuwania Urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, wakazi wengi wa jimbo hilo wana imani kwamba 'anatosha' kuliongoza taifa hili.
 
 Wazungumzaji ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimboni humo, wanamuelezea Lowassa kama mwanasiasa anayestahili 'kumrithi' Rais Jakaya Kikwete.  
 
"Lowassa ni chaguo sahihi kwa sasa na sio wakati mwingine…hii inatokana na sifa za uongozi ambazo anazo na uzoefu alioupata katika utumishi wake," anasema Reuben Ole Kuney, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Monduli.
 
Anataja baadhi ya sifa za Lowassa kuwa ni mtu mwenye akili na hana woga kutumia akili zake kupambana na umaskini unaokithiri. 
 
 "Huyu ndiye anayejua tumeanguka wapi na tunatakiwa twende wapi," anasema na kuogeza, "anaijua nchi yake, anaielewa na hababaishi kama ilivyokuwa kwa wengine."
 
  Hata hivyo, wanaompinga Lowassa wamekuwa wakitumia kumbukumbu za kashfa za ufisadi hususani iliyo maarufu kama 'kashfa ya Richmond' na kuhoji vyanzo vya utajiri wake kuwa ni miongoni mwa mambo yanayomfanya akose sifa za kushika wadhifa huo. 
 
Lakini Ole Kuney anasema, "Lowassa hana tabia ya ugomvi na mtu lakini wapo baadhi wanaomhofia kwamba akiwa Rais, atalipa kisasi – cha nini hasa? Huko ni kumpaka tu matope bure, labda wao wanajua nini wametendea."
 
 Anaongeza, "apewe nafasi na kwa muda mfupi tu watu wataona nchi inavyobadilika na kupiga kasi kubwa ya maendeleo."
 
 Kwa mujibu wa Ole Kuney, imedhirika kwamba wakazi wa Monduli  wanamjua na kumpenda Lowassa na kwamba hata ingefaa akashika nyadhifa za Urais na ubunge kwa wakati mmoja, ingewezekana na angeungwa mkono na CCM na wapiga kura wake.
 
Ole Kuney, anamtaja Lowassa kama kiongozi aliyejiandaa kupambana na umaskini uliokithiri miongoni mwa watu, huku akishangaa kuona hata nchi ndogo (anazitaja) zinaipita Tanzania kwa maendeleo. 
 
Anasema kuwa kwake karibu na Lowassa kumempa fursa ya kujua moja ya fikra zake (Lowassa) katika kupambana na umasikini ni uboreshaji wa elimu ili sekta hiyo ilete ufanisi katika kuifanya jamii iondokane na ujinga.
 
 Anasema, Lowassa ni mtu ambaye akipewa kazi anaifanya kwa uaminifu mkubwa, kwa kufuatilia na kwa ujumla anapenda vitu vyake vionekane vimekamilika kwa viwango.
 
 Ole Kuney anasema kwa kipindi alichokuwa karibu na Lowassa, amebaini kuwa ni kiongozi asiyependa udanganyifu na ulaghai.
 
 "Hapendi tabia ya watu kutosema ukweli wa jambo, iwe kwenye ripoti au katika mazungumzo…anapenda mtu awe anajiamini na kuwa makini, hapendi kuona watu hawabadiliki ki-maendeleo," anasema. 
 
Anasema mara nyingi, Lowassa amekuwa akihoji inakuwaje tangu Tanzania ipate uhuru Desemba 9, 1961 hadi sasa, maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umasikini aliowataja Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hawajaondolewa kwa Watanzania.
 
 ALIVYOMFAHAMU LOWASSA
Anasema alimfahamu Lowassa wakati akisoma Middle School wakati yeye (Ole Kuney) alikuwa sekondari ambapo wazazi wao walikuwa wanafanya kazi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Monduli, enzi za utawala wa kikoloni. 
 
"Tulikuwa tunashirikiana kwa mengi kama kuchunga ng'ombe na kulima…wakati fulani nilikuwa ninamfundisha na nikawa mwalimu wake…Lowassa alikuwa mwadilifu, nadhifu na kiongozi wa bendi ya shule," anasema.
 
 Wakati Ole Kuney akienda kusomea ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walipewa kazi kila mwanachuo amtafute mwanafunzi wa shule ya msingi ili kumfuatilia maendeleo yake kimasomo na kisha kuandika taarifa maalum. 
 
Anasema alimchagua Lowassa na kumfuatilia (study) pamoja na wazazi wake. Anasema kazi hiyo ya ufuatiliaji aliyohitimisha kwa kuandika taarifa maalum katika somo lake la ualimu aliifanya vizuri kiasi cha kupata daraja A na huo ulikuwa mwaka 1968.  
 
DADA: NYOTA ILING'ARA TANGU UTOTONI
Kalaine Lowassa (68) ni dada mkubwa wa Lowassa (Edward) ambaye anasema hana wasiwasi na uwezo wa Mbunge huyo kuliongoza Taifa.
 
"Kutokana na uwezo wa kuongoza wenzake (Lowassa) akiwa bado mdogo, utendaji na uzoefu wake wa kazi nina imani kwamba anaiweza kazi ya Urais ikiwa atapitishwa na CCM na kuchaguliwa na Watanzania," anasema.
 
 Anasema walipokuwa katika marika ya utoto na ujana, Lowassa (Edward) alikuwa na ujasiri wa kumueleza baba yao jambo lolote kwa ufasaha, kwa niaba ya wenzake na mzazi wao huyo akawatekelezea. 
 
Anatoa mfano kama wao walikuwa wanashida ya fedha, walikuwa wakimtuma Lowassa akawaombee kwa baba yao. 
 
 "Mimi nikiwa dadake namjua tangu akiwa mtoto, anaweza kuongoza, nyota yake ya ujasiri na kuwaongoza wengine ilionekana tangu utotoni, ingawa alikuwa mdogo lakini alisaidia kufanyika kwa mambo mengi kuliko hata ilivyochochewa na wakubwa wake," anasema.
 
 "Siyasemi haya kwa sababu tu ni mdogo wangu, hapana. Kila mtu, vijana kwa watu wazima wanasema Lowassa anaweza. Ukitaka kuthibitisha hilo pita mahali po pote watu wamempima na kuona anaweza kuiongoza Tanzania," anasema. 
 
Kalaine anasema tangu akiwa mtoto, Lowassa hakuwa na hulka ya kuchagua kazi za kufanya kutokana na kupenda kufanya kazi zote na kujituma. 
 
Lakini pia anasema familia yao (wazazi) ilikuwa na utaratibu mzuri wa kutupangia kazi zote za nyumbani, hivyo aliweza kufanya kazi za kilimo, kuchunga ng'ombe na zingine alizopangiwa.
 
"Akiwa kijana mdogo, Lowassa alishiriki kuchunga ng'ombe na wakati mwingine kumsaidia mama kazi za nyumbani na za mashambani, hakuwa anachagua kazi. Hata alipokuwa Chuo Kikuu, wakati wa likizo aliporudi nyumbani alienda kuchunga," anasema. 
 
Pamoja na dada wa mbunge huyo, Kalaine ni mpiga kura katika jimbo la Monduli, anayeamini kuwa Lowassa amefanikisha kuwapo kasi kubwa ya maendeleo, ustawi wa watu na huduma za kijamii kama shule, maji, hospitali na barabara.
 
 Ndio maana anaamini kwamba kama Lowassa asingepata 'ajali ya kisiasa' na kuutumikia wadhifa wa Waziri Mkuu kwa awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Kikwete, kungekuwa na mabadiliko makubwa katika nyanja tofauti za maendeleo nchini.
 
AFISA TARAFA ANENA 
Afisa Mtendaji wa Tarafa ya Kisongo, Paulo Kiteleki huko Monduli ana amtaja Lowassa kuwa ni mchapaka kazi, mwadilifu na mwenye kutoa uamuzi mgumu katika masuala yanayouhusu umma wa Watanzania.
 
 Anasema moja ya viashiria vya utendaji kazi bora wa Lowassa, ni namna alivyofanikisha kuanzisha Mfuko wa Vijana wenye 'hazina' ya zaidi ya shilingi milioni 300.
 
Mfuko huu uliojulikana kama 'Vijana Maisha Bora Fund' ulianzishwa jimboni humo kwa lengo la kusaidia vijana.
 
Vijana wengi walianza kunufaika na mfuko huo kwa kuanzisha vikundi vya watu watano kila kata na kubuni miradi ya kufanya kama vile katika kikundi kununua ng'ombe na kuuza na wengine walinunua na kuwauza mbuzi.
 
Anasema kuanzishwa kwa mfuko huo kulitokana na umuhimu wa kuwasaidia vijana, hivyo karibu kila kata (vijana) waliunda vikundi hivyo na kuchangia fedha kabla ya kuanza kukopa kwa ajili ya miradi. 
 
Fedha hizo zinarejeshwa kwa utaratibu mahususi ili kutoa fursa kwa vijana zaidi kukopa.
 
"Monduli inamuona Lowassa kuwa anaweza kufanya mambo makubwa sana katika nchi hii," anasema Afisa Mtendaji huyo na kuongeza, "kama Watanzania tutapewa fursa ya kumchagua Lowassa na akapitishwa bila mizengwe, Tanzania itakuwa imepata Rais bora na si bora Rais." 
 
 Mkazi wa Monduli, John Ngao Kimati (80) anasema amemfahamu tangu mwaka 1964, wakati akisoma Monduli Middle School Moringe na kwamba ni kiongozi mzuri.
 
 "Akichaguliwa tu ndani ya CCM, kwa wananchi atapita kweupe. Hata huko Moshi wanasema huyu amekwishapita tayari," anasema na kuongeza, "mtihani mkubwa kwake upo CCM, kwa wananchi ni mteremko." 
 
Makamu Mwenyekiti wa viongozi wa mila wa kabila la Wamasai wilayani Monduli, (malaigwanani), Mepukori Mberekeri kutoka kijiji cha Mti Mmoja, anasema wamemchagua Lowassa kuwa Laigwanani Mkuu kutokana na ujasiri wake katika kuwatumikia wananchi.
 
 "Anaweza, hata malaigwanani wamemchagua kuwa kiongozi wao hapa nchini. Kwa upande wetu mtu mpaka achaguliwe kuwa kiongozi wa nafasi hiyo ujue amechujwa na kuona anafaa kuwa kiongozi," anasema. 
 
Anasema hata ukienda pale nyumbani kwake, haijapata kutokea hapa kwetu kiongozi wa aina yake kupokea makundi ya watu wanaomtembelea kila siku.
 
 SHULENI KWAKE
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Moringe,  ambayo awali ilijulikana kama Monduli Middle School, Ndesamburo Kwayu, pamoja na msaidizi wake, Simon Panga, wanasema Lowassa ni kiongozi anayefaa kutokana na sababu kadhaa ikiwamo kauli anazotoa zinalingana na matendo yake.
 
 "Ingawa sikumfundisha, nilisikia alikuwa mtanashati, kiongozi wa mdahalo na kiongozi wa bendi ya  shule."
 
 "Amekuwa kiongozi wangu hapa akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hii kwa muda mrefu na kipindi chote alikuwa karibu sana na shule na hata baada ya kumaliza muda wake mara kwa mara amekuwa akija kutupongeza pale tunapofanya vizuri katika mitihani ya taifa," anasema.
 
 Anasema amemfahamu Lowassa miaka 30 iliyopita akiwa anafundisha shuleni hapo na kwamba jamii ya shule hiyo inajivunia kuwa na watu maarufu waliosoma hapo wakiwamo hayati Edward Moringe Sokoine na Lowassa.