MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za mfululizo zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zitaendelea kunyesha na kwamba zinatarajia kupungua mwishoni mwa wiki hii.
Taarifa hiyo inaweza kuwa habari njema kwa wakazi wa Dar es Salaam na miji mingine iliyoathirika kwa kiasi kikubwa na mvua hizo zilizonyesha mfululizo na kusababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu, huku hali ya usafiri, upatikanaji wa bidhaa hasa za vyakula ikiwa ngumu katika maeneo mengi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Jamii wa TAM, Hellen Msemo alisema mvua hizi zinatarajia kupungua mwishoni mwa wiki hii; lakini sio kuisha kabisa na kwamba kwa sasa wananchi waendelee kufuatilia taarifa zinazotolewa.
"Mvua hizi zitaendelea kunyesha mpaka Ijumaa ya wiki hii na tunaweza kuona jua kidogo Jumamosi lakini sio mvua za kukatika kabisa zitaendelea kunyesha kidogo kidogo," alisema Msemo.
Shule zajaa maji
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani 'B', Jane Reuben alisema mvua zinazoendelea kunyesha zimeathiri kwa kiasi kikubwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni hapo huku wengine wakichelewa kufika darasani.
Gazeti hili lilishuhudia hali tete katika shule ya Msingi Msasani 'A' ambapo baadhi ya madarasa yamejaa maji na kushindwa kutumika na kuwalazimu wanafunzi kuchangia vyumba vya madarasa.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi wanaosoma katikati ya jiji wameshindwa kufika shuleni kwa kuhofia usumbufu wa usafiri kutokana na mvua ambayo imekuwa ikiendelea kunyesha.
Baadhi ya shule katika Kata ya Goba zimefungwa kwa muda kutokana na athari za mvua hizo. Foleni zawa kero Mvua hizo pia zimeendelea kuleta usumbufu mkubwa katika barabara nyingi za Dar es Salaam kutokana na kuharibika na kusababisha msongamano unaowafanya wakazi wa jiji hilo kupata wakati mgumu wa kuyafikia maeneo mbalimbali ama kikazi au shughuli binafsi.
HabariLeo ilishuhudia maeneo ya Posta Mpya katika barabara za Samora Avenue, Mkwepu, Ocean Road, Uhuru na zile zinazoelekea Magomeni na Mwenge zikiwa na msongamano wa magari.
Bidhaa bei juu Kwa upande wa bidhaa katika masoko, bei zimepaa na kusababisha kuongezeka kwa ukali wa maisha miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam.
Katika soko la Kariakoo, mfanyabiashara Baraka Lisulile anayeuza karoti alisema kabla ya mvua kilo moja ilikuwa inauzwa kwa Sh 2,000 lakini sasa imefikia Sh 3,000.
"Vile vile kabla ya mvua hizi kunyesha tenga la nyanya lilikuwa ni kati ya Sh 20,000 hadi Sh 35,000 lakini hivi sasa ni kuanzia Sh 48,000 hadi Sh 50,000," alisema mfanyabiashara huyo.
Bidhaa za unga, mchele, maharage na aina nyingine za vyakula, nazo ziko juu. Nyumba zabomoka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Musa Natty alisema mvua hizo zimefanya wananchi kukumbwa na uharibifu mkubwa ambao ni nyumba kufurika maji, kubomoka na barabara na madaraja kukatika.
Alisema katika manispaa hiyo maiti nne za wanaume na mwanamke moja zimepatikana na zimeripotiwa kata za Wazo Kunduchi na Mbezi beach.
Katika manispaa hiyo pia eneo la Africana nyumba zimejaa maji huku maeneo ya Nyaishozi kaya 151 zinahitaji msaada wa haraka ikiwemo mahema na chakula.
Alisema kata ya Tandale maeneo ya bondeni maji yameingia katika mitaa ya Pakacha, kwa Tumbo, Mahalitani, Sokoni, Mtogole na kwa Mkunduge.
Nyumba 14 ndizo zilizoathirika kwa kubomoka ambapo wakazi wake wamehifadhiwa na majirani.
Kata ya Kwembe watu 23 wamepata majeraha baada ya nyumba kuezuliwa paa, Shule ya Msingi King'azi ambayo inamilikiwa na Manispaa nayo imepata maafa ya kutitia na kutoa ufa kati ya lenta na paa.
Kata ya Mbweni familia 128 zimeathirika kwa kuzungukwa na maji na kukosa makazi na kuhifadhiwa na majirani na kata ya Magomeni mwili wa mtu mmoja umeopolewa akiwa amekufa, katika mtaa wa Suna watu 450 wamekosa makazi na mtaa wa Makuti A watu 250 hawana makazi na wanahifadhiwa na majirani.
Mtaa wa Idrisa watu 180 hawana makazi na nyumba nyingine 450 kuzingirwa na maji Kata ya Mabwepande daraja la mto Nyakasangwa mtaa wa Mbopo limekatika na kutitia hakuna mawasiliano kati ya pande mbili na barabara ya kwenda Mabwepande imekatika karibu na njia panda iendayo kwa waathirika wa Mji Mpya na nyumba 20 zimezingirwa na maji.
Kata ya Hananasif nyumba 400 ambazo ziko mabondeni zimezungukwa na maji na wakazi wa nyumba hizo wamehama makazi yao. Nyumba hizo ni zile zilizopo bondeni ambazo zilizobaki baada ya kubomolewa na wamiliki kupelekwa Mabwepande.
Kata ya Mabibo daraja la Tasaf linalounganisha Kata ya Mabibo na Makuburi limekatika kwa sababu ya wingi wa maji pamoja na nyumba tisa na vyoo.
Kata ya Manzese kumeripotiwa kifo cha mtu mmoja na kubomoka kwa nyumba moja. Daraja la linalounganisha kata ya Mbezi juu kwa Londa na Makongo kukatika.
Kata ya Wazo mtaa wa Mivumoni nyumba 13 zimeezuliwa na upepo mkali na Kata ya Kawe Mtaa wa Mzimuni nyumba 64 zimebomoka na nyingine kuzunguka na maji.
Kata ya Makumbusho mwili wa mtu mzima miaka 45 umeokotwa na waathirika 109 waliobomokewa na nyumba na zingine kujaa maji wamehifadhiwa shule ya msingi Kisiwani ambao wanahitaji msaada.
Kata ya Msasani Shule ya msingi msasani A imejaa maji katika madarasa 7 na nyumba za walimu na shule imefungwa kwa muda, Kata ya Sinza maji yamejaa yanaelekea katika makazi ya watu huku mtaa wa Barafu nyumba 3 zimebomoka na watu kukosa makazi huku nyumba 275 zimezungukwa na maji na kuhatarisha makazi.
Kata ya Mwananyamala katika mitaa ya Msisiri A na Msisiri B, Bwawani na mtaa wa Mwinyijuma jumla ya nyumba 150 zimezingirwa na maji na kuleta taabu kwa wakazi wake.
Kata ya Makuburi nyumba mbili zimebomoka na daraja la waenda kwa miguu linalounganisha Kata za Makuburi na Kimara kusombwa.
Kata ya Kimara familia saba zimehamia katika Kituo cha Polisi cha Kilungule A baada ya nyumba yao kujaa maji na kukatika, Kata ya Mizimuni nyumba tano zimevunjika kuta na kaya 15 zimehamia kwa majirani huku kaya 30 nyumba zake zimezingirwa na maji.
Kufuatia maafa hayo, Halmashauri imechukua jitihada mbalimbali ili kuokoa maisha ya watu na kuwawezesha kurudi katika makazi yao. Jitihada hizo ni pamoja ni kununua pampu za kunyonya maji ambayo yamezunguka makazi ya watu.Kazi hiyo ya kunyonya maji imeanza pamoja na kuzibua mitaro.
Imeandikwa na Regina Kumba, Lucy Ngowi na Emmanuel Ghula