Friday, May 15, 2015

Albino mwingine akatwa mkono



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi,            Dhahiri KidavashariKamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari





Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari

MWANAMKE mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Remi Luchoma (30), mkazi wa kijiji cha Mwamachoma kata ya Mamba wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi, amekatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana, kisha wakatokomea na kiganja cha mkono huo kusikojulikana.
Kwa sasa, mtu huyo amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa alithibitisha kumpokea mama huyo na kwamba anapatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Alieleza kuwa tukio la kukatwa mkono wa albino huyo, lilitokea hapo jana majira ya saa 6 usiku nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji hicho.
Alisema baada ya kukatwa kiganja chake cha mkono wa kulia, albino huyo alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Mamba, ambapo alipewa rufaa na kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda kwa ajili ya matibabu zaidi.
Alipokewa katika hospitali hiyo ya wilaya saa 10 alfajiri na amelazwa wadi namba mbili .Hali yake inaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Masuma Luchuma ambaye ni kaka wa albino huyo, alisema tukio hilo la dada yake kukatwa kiganja cha mkono ni la kinyama na limemsikitisha. Alisema tukio hilo lilitokea kwenye chumba alichokuwa akiishi albino huyo, mwenye watoto wanne.
Kaka huyo alisema siku ya tukio majira ya saa 6 usiku, alisikia watu wakivunja mlango wa chumba alichokuwa amelala Remi na baada ya muda mfupi, alisikia dada yake huyo akipiga mayowe ya kuomba msaada.
Alidai alijaribu kutoka nje ili kumwokoa dada yake huyo, lakini alishindwa kutoka nje kwa kuwa watu hao walifunga mlango wake kwa nje. Alisema hali ya kufungiwa ndani, ilimfanya apige kengele ya jembe, kama ishara ya kuomba msada kwa majirani .
Hali hiyo iliwafanya watu hao, wakimbie na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na msako mkali kuwasaka waliohusika na tukio hilo.