Wednesday, April 01, 2015

VIONGOZI WA DINI WAJITOSA MGOGORO WA WAFANYABIASHARA NA TRA



VIONGOZI WA DINI WAJITOSA MGOGORO WA WAFANYABIASHARA NA TRA
 
Kamati ya Maadili ya Amani na Haki za Binadamu ya madhehebu ya dini  nchini imemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzungumza na wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua mgogoro uliopo baina yao.

Kauli hiyo imekuja baada ya wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo kugoma kufungua maduka yao wakilalamikia ujio wa mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD).
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Askofu William Mwamalanga alisema jana kuwa wamegundua mgogoro huo una lengo la kuhujumu maendeleo ya Watanzania.
"Kufunga biashara kwa siku tano ni jambo ambalo halikubaliki katika nchi inayojitutumua kujitegemea," alisema Askofu Mwamalanga.
Katika tamko hilo, maaskofu na masheikh walimtaka Waziri Pinda kuwawajibisha baadhi ya watendaji wa Serikali wanaodaiwa kutumia madaraka yao kukuza mgogoro huo.
 "Viongozi wa dini ili tujenge nyumba za ibada, hospitali, shule na miradi ya maji kwa jamii tunahitaji biashara," alisema  Askofu Mwamalanga.
Katika hatua nyingine; Mjumbe wa kamati ya kitaifa ya kushughulikia vikwazo vya kibiashara visivyo vya forodha, Jimmy Mwalukelo alisema mgogoro huo unazorotesha uchumi.
"Kosa walilofanya TRA ni kupeleka mashine moja kwa moja kwa wafanyabiashara bila kutupa elimu mawakala wao ambao ndiyo tunaowapelekea wateja wetu.
"Mteja akitaka kwenda kulipa kodi ni lazima muhasibu amfanyie hesabu ndiyo aende kulipa kodi za ndani," alisema Mwalukelo.