SERIKALI iko mbioni kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa ardhi hapa nchini, utakaosaidia kupima, kupanga na kukusanya kodi ya pango la ardhi na kuondoa kero ambazo wananchi wamekuwa wanakumbana nazo katika sekta hiyo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alibainisha hayo jana katika Ukumbi wa Karimjee alipozungumza na watumishi wa sekta ya Ardhi wa Wizara pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Lukuvi alieleza kuwa kumekuwepo na matumizi mabaya ya madaraka kwa watumishi wa sekta ya ardhi, hivyo kusababisha kero kwa wananchi na wananchi kuporwa ardhi ambayo ni haki yao.
Aidha, Lukuvi alisema mfumo mzima na utaratibu wa uendeshaji na uwekaji wa kumbukumbu katika sekata ya ardhi, hauridhishi na unatoa nafasi kubwa kwa watumishi katika sekta hiyo kukiuka taratibu nyingi, ikiwemo kutowahudumia wananchi kwa haraka na kwa muda unaotakiwa pamoja na matumizi mabaya ya lugha.
"Watumishi katika sekta hii wamekuwa hawaweki kumbukumbu za nyaraka wanazofanyia kazi,kuna matumizi mabaya ya madaraka, barua hazijibiwi kwa wakati pamoja na baadhi ya watumishi kujimilikisha viwanja vingi wakati baadhi yao hawana viwanja," alisema Lukuvi na kuongeza kuwa kumekuwepo pia na tabia ya watumishi kuficha viwanja na kuwaelekeza watu viwanja vya mabondeni.